Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amemuagiza Mkandarasi M/s China Geo-Engineering Corporation kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara kiwango cha lami Km 10.21, mtaro wa maji ya mvua Ilazo Km 2.1, uboreshaji wa mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua (3), mitaro ya kutiririsha maji Km 2.81 pamoja na ujenzi wa jengo la usimamizi na uratibu wa miradi kwa wakati na ubora.
Mhandisi Mativila ametoa agizo hilo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo jijini Dodoma ambayo inatekelezwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC) chini ya mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Naibu Katibu Mkuu ameeleza kuwa baada ya ukaguzi wa mradi huo amebaini kuwa ujenzi wa barabara, mifereji ya maji ya mvua pamoja na jengo la usimamizi na uratibu wa miradi upo nyuma ya muda kutokana na nguvu kazi hafifu, ukosefu wa vitendea kazi na kupelekea mradi huo ambao unapaswa kukamilika Februari 2025 kuonyesha ishara za kutofikia malengo ya kukamilika kwa muda na kuwanyima wananchi fursa ya kupata huduma ya barabara.
“Mradi upo asilimia 45% tu bado zimebaki 55% kazi kukamilika, mpaka leo zimebaki siku 13 tu ili mkataba ukamilike. Tumeongea na mkandarasi lakini tumeona sehemu kubwa ya ucheleweshaji wa kazi umesababishwa na mkandarasi mwenyewe kwa kushindwa kuweka nguvu kazi na vifaa vya kutosha, ametueleza anahitaji mwaka mwingine ili akamilishe kazi kiukweli ataongezewa muda lakini atapata adhabu ya kukatwa fedha kulingana na mkataba na pia atatakiwa afanye kazi usiku na mchana ili akamilishe kazi ndani ya muda mfupi na kwa ubora ule ule”. amesema