Featured Kitaifa

ANWANI ZA MAKAZI KUCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI-MAJALIWA

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa akizungumza katika  Kilele cha Maadhimisho ya Wiki  ya Anwani za Makazi kwenye  Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

 ….

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema mfumo wa anwani za makazi utasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi, kuharakisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama, kuwezesha biashara mtandao kufanyika kwa ufanisi na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 8, 2025) katika maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Anwani za Makazi yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Katika kilele hicho Waziri Mkuu amezindua matumizi ya mfumo wa Anwani za Makazi. Kaulimbiu za maadhimisho hayo inasema “tambua na tumia anwani za makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma”.

Waziri Mkuu amesema suala la anwani za makazi ni moja ya masuala yaliyopewa kipaumbele katika Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2021/2022- 2025/2026 ambao umeweka bayana azma ya Serikali ya kujenga mfumo wa anwani za makazi na postikodi katika kata zote nchini.

“…siku kama ya leo tarehe 8 Februari, 2022, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi nchini kwa njia ya operesheni. Operesheni hiyo ilifanyika kwa muda wa miezi minne na kuwezesha ukusanyaji wa taarifa milioni 12.3 za anwani za makazi zilizohifadhiwa katika mfumo wa kidijitali wa anwani za makazi unaojulikana kwa jina la National Physical Addressing (NaPA).

Amesema kupitia programu ya NaPA mwananchi akiwa eneo lolote nchini na hujui sehemu ya kupata huduma za kijamii kama vile kituo cha afya au mgahawa anaweza kutumia programu hiyo kutafuta sehemu za karibu. “Hii ni programu bora na inarahisisha kupata huduma husika sambamba na kwenda na kasi ya kimaendeleo katika uchumi wa sasa wa Kijiditali.”

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kutunza na kuwa walinzi wa miundombini ya anwani za makazi kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa katika kugharamia miradi hiyo. “Vibao tulivyoviweka kuonesha mitaa na barabara, tunao Watanzania ambao si waaminifu wanang’oa mabago hayo na kwenda kuyauza, ni muhimu kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo kwa sababu inamanufaa.”

Kwa upande wake, Waziri Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kusimamia na kuendeleza miundombinu na mifumo ya msingi (Foundation Systems), ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa kidijitali ulioainishwa katika Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Miaka 10 (2024–2034).

Amesema mifumo hiyo inajumuisha mifumo ya utambuzi wa watu, biashara, ardhi, na makazi. “Katika muktadha huu, utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni hatua ya kimapinduzi inayolenga kuboresha utambuzi na utoaji wa huduma kwa wananchi hapa nchini.”

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nadir Abdulatiff Awady amesema zoezi la uwekaji wa anwani za makazi kwa upande wa Zanzibar limekamilika kwa asilimia 100, ambapo kwa sasa wanaendelea kuwahamasisha wananchi matumizi ya anwani hizo.

Awali, Naibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt, Festo Dugange alisema kabla ya utekelezaji wa mfumo huo ilikuwa ni vigumu kwa mgeni kufika katika baadhi ya maeneo ila kwa sasa imerahisishwa baada ya utekelezwaji wa mpango huo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa  Pharles Ngelea, Mhandisi Mshauri wa TARURA Makao Makuu kuhusu shughuli zinazofanywa na TARURA katika kufanikisha suala zima la Anwani za Makazi wakati alipotembelea mabanda ya maonesho kabla ya kuzungumza katika Maadhimisho ya  Wiki ya Anwani  za Makazi kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025.   Wa pili kulia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa na  wa tatu kulia ni Naibu Waziri TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha  Mawasiliano Serikalini TAMISEMI, Nteghenjwa Hossea na wa tatu kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TARURA  Makao Makuu, Catherine Sungura. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza, Agnes Gerald, Afisa Habari Mwandamizi Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka hiyo kabla ya kuzungumza  katika Maadhimisho ya Wiki ya Wiki ya Anwani za Makazi kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025. Kulia kwake ni Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama pikipiki inayotumika kusambaza barua na vifurushi kwa maa wa Anuani za Makazi alipotembelea banda la monesho la Shirika la Posta  Tanzania  kabla ya kuzungumza  katika Maadhimisho ya Wiki ya Wiki ya Anuani za Makazi kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa,akizungumza katika  Kilele cha Maadhimisho ya Wiki  ya Anwani za Makazi kwenye  Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa akizungumza katika  Kilele cha Maadhimisho ya Wiki  ya Anwani za Makazi kwenye  Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Baadhi ya viongozi walioshiriki katika Kilele cha Maadhimisho ya  Wiki ya Anwani za Makazi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza  kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa akipokea kwa naiba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tuzo ya kutambua na kuthamini Mchango wa Rais katika kuimarisha masuala ya utambuzi nchini kupitia oparesheni ya  Anwani za Makazi ya 2022. Makabidhiano hayo yalifanyika katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa akionesha tuzo aliyoipokea kwa naiba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutambua na kuthamini Mchango wa Rais katika kuimarisha masuala ya utambuzi nchini kupitia oparesheni ya  Anwani za Makazi ya 2022. Makabidhiano hayo yalifanyika katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya  Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe wakati alipozindua utoaji wa huduma za barua za utambulisho wa njia  ya kidijitali na utoaji wa Vishikwambi katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Februari 8, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

About the author

mzalendoeditor