Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amekosoa utaratibu unaotumika wa abiria kuingia na kutoka stesheni kuu ya treni ya mwendokasi (SGR) Dodoma, kuwa umekuwa ukileta adha kwa abiria, hivyo ametoa maagizo kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma na Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha ndani ya siku saba wanabadilisha utaratibu huo.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo Februari 6, 2025 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa Ujenzi wa Soko Kuu la Majengo pamoja na ujenzi wa kituo cha daladala eneo la Mshikamano Kizota na Nzuguni.
“Ninawataka Wakurugenzi wote wa majiji lakini hasa Jiji hili la Dodoma ndiyo Makao Makuu ya Nchi, Mkuu wa Mkoa, Wilaya nendeni mkajipange hasa pale eneo la stesheni ya rel, utaratibu wa watu kuingia na kutoka haujakaa vizuri, nendeni mkakae pamoja na TRC muweke utaratibu mzuri, haieleweki, Rais hawezi kutuelewa”, amesema.
Aidha, Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo kuhakikisha kuwa sheria ya kuanzishwa kwa Makao Makuu ya nchi inaharakishwe kuingia Bungeni kabla ya kuvunjwa kwa Bunge hili.
“Tutapeleka hati ya dharura bungeni ili kuhakikisha sheria hiyo inapitishwa ya kuhakikisha sheria hiyo ya kuanzishwa makao makuu inapitishwa ili dhamira ya Dodoma kuwa makao makuu iwepo kwenye sheria,” amesisitiza Mchengerwa
Pia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA kutowapa Zabuni wakandarasi ambao hawatekeleza miradi badala yake ahakikishe wamekamilisha miradi yote ili ikawasaidie wananchi.
“Asitokee mkandarasi ambaye hajakamilisha Mradi atakayepewa mradi mwingine ndani ya TARURA nchi nzima maana kuna wakandarasi Wana miradi mingi na hawajaikamilisha sasa maelekezo yangu sitaki kuona mkandarasi akipataka kazi nyingine wakati Ana kiporo hajakikamilisha, “ameeleza Mchengerwa
Kwa upande wake Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema hawalizishwi na namna mkandarasi anayetekeleza mradi huo awamu ya kwanza anavyofanya kazi kwani hawatendei haki na tayari fedha kiasi cha Bilioni 24 amekabidiwa kwaajili ya utekelezaji.
“Anatakiwa akabidhi mradi huu Februari 19 mpaka leo ukimuuliza asilimia alizozifikia ameshindwa kufika hata 50% katika baadhi ya maeneo Barabara ya kutoka Mkalama kwenda Ntyuka hajakwenda kwa kasi tuliyoitegemea,”amesema.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TACTIC katika Jiji la Dodoma Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema kuwa mradi unatekelezwa kwa awamu mbili katika Halmashauri zote 12 ikiwemo Jiji la Dodoma.
“Awamu ya kwanza utekelezaji ulianza na Barabara na Mifereji ya maji ya mvua ambapo Mikataba ilisainiwa kwa pamoja tarehe 23/09/2023 na Makandarasi walianza utekelezaji tarehe 20/11/2023 kwa mikataba ya Miezi 15 ambapo imepangwa miradi kukamilika ifikapo tarehe 19/02/2025,”amesema.
Amesema Miradi inayoendelea ya awamu ya kwanza ni ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kilomita 10.21, Mtaro wa maji ya Mvua Ilazo kilomita 2.1, Uboreshaji wa Mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua (3) na mitaro ya kutiririsha maji Kilomita 2.81 na ujenzi wa jengo la usimamizi na uratibu wa miradi.
“Katika Jiji la Dodoma, miradi itakayotekelezwa awamu ya 2 ya kundi la kwanza ni uboreshaji wa Soko kuu la Majengo pamoja na kituo cha daladala eneo la Mshikamano, uboreshaji wa Stendi ya mabasi madogo eneo la Kizota, ujenzi wa Stendi ya mabasi madogo eneo la Nzuguni na ujenzi wa Vivuko vya Maji (Footbridges) katika maeneo ya Chaduru, Maili Mbili na Ntyuka,”amesema.