Featured Kitaifa

UANDIKISHAJI WA WANAFUNZI UFANYIKE BILA KUJALI TOFAUTI ZAO’ MHE MCHENGERWA

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaagiza viongozi wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha uandikishaji wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari unafanyika bila kujali tofauti zao za kiafya na kimaumbile.

Ametoa maagizo hayo leo Januari 6, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi vyumba 18 vya madarasa vilivyogharimu sh Milioni 300 katika halmashauri ya wiaya ya Bahi na utoaji tuzo kwa waandishi wa habari za mradi wa shule bora 15.

Amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanasimamia zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wote bila kujali tofauti zao za kiafya na kimaumbile wenye umri lengwa kwa ajili ya kuanza darasa la Awali, darasa la kwanza na MEMKWA

‘Nawaagiza mkasimamie kwa dhati zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wote bila kujali tofauti zao za kiafya na kimaumbile wenye umri lengwa kwa ajili ya kuanza darasa la awali msingi na MEMKWA’ amesisitiza

Amewataka kuhakikisha wanasimamia kwa dhati uripoti wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka wà masomo 2025

Mchengerwa amewataka viongozi hao kutoa takwimu sahihi za uandikishaji na uripoti wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Kila siku ya Ijumaa katika wiki).

Vilevile ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, kuhakikisha inatunza miundombinu ya vyumba vya madarasa yaliyokabidhiwa ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

Kuhusu mradi wa shule bora Mchengerwa amesema mradi huu ulizinduliwa rasmi na Vicky Ford (Parliamentary Under Secretary State-UK) Aprili 4, 2022 katika shule za Msingi Mkoani iliyopo Kibaha- Pwani ukiwa ubeba lengo kuu la kuboresha ujifunzaji na ufundishaji katika ngazi ya Elimu ya Awali na Msingi katika Mikoa tisa Tanzania Bara.

Amesema uteuzi wa mikoa hiyo ambayo ni Dodoma,Singida,Pwani,Tanga, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa ulizingatia mambo mbalimbali ikiwemo ufaulu usioridhisha wa wanafunzi katika mitihani ya kuhitimu darasa la saba na ile ya upimaji wa darasa la Nne, utoro, mimba za utotoni.

“Hivyo, uwepo wa mradi huu ni sehemu ya tiba ya kutibu changamoto hizo ili kuweka mizania ya hali ya utoaji wa elimu kwa kila mtoto mwenye umri wa kuanza na kumaliza shule.”

Aidha Mchengerwa alisema kwa kipindi cha miaka mitatu (2022-2024), umejikita katika kuboresha elimu ngazi ya elimu ya awali na msingi kwa kuangazia maeneo manne ambayo ni ujifunzaji, ufundishaji, ujumuishi na uimarishaji wa mifumo ambapo shughuli mbalimbali zimefanikiwa kutekelezwa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu ambayo yameleta matokeo makubwa ikiwemo kuongeza ufaulu Dodoma kwa shule za msingi na sekondari na kupunguza utoro kutoka wanafunzi 24000 hadi 6000(2024).

Akitoa taarifa kuhusu umalizaji wa ujenzi owa madarasa hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi, Zaina Mlawa alisema ujenzi wa omadarasa 10 kwa kufuata mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji una lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Mwakilishi wa Balozi kutoka ubalozi wa Uingereza, Sally Hedley alisema elimu ni kipaumbele kwa serikali hiyo hivyo nchi hiyo itaendelea kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuweka miradi rafiki ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wanafunzi.

Amewataka viongozi hao kutoa takwimu sahihi za uandikishaji na uripoti wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya awalina msingi.

About the author

mzalendo