Featured Kitaifa

RAIS SAMIA: CCM ITALETA WAGOMBEA WANAOKUBALIKA

Written by mzalendoeditor

_Mwenyekiti wa CCM aahidi mchujo wa haki kwa wagombea 2025_

_Mawazo ya wananchi kuzingatiwa ili kuimarisha ushindi kwa chama_

Dodoma, tarehe 5 Februari 2025

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa CCM italeta wagombea wanaokubalika na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, ili kurahisisha uchaguzi wa diwani, mbunge na rais kutoka chama hicho.

Akizungumza leo katika kilele cha sherehe za miaka 48 ya CCM, zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Dkt. Samia alisisitiza kuwa mchakato wa kupata wagombea utazingatia haki na uwazi, kwa kushirikiana na viongozi wenzake ndani ya chama.

“Nawahakikishia wana-CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa, tutahakikisha haki inatendeka katika mchakato wa kupata wagombea wa CCM. Lengo letu ni kuleta wagombea wanaokubalika, ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya kuchagua mafiga matatu—diwani, mbunge, na rais,” alisema huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi.

Kwa upande wa Zanzibar, alieleza kuwa mwelekeo huo utahakikisha upatikanaji wa diwani, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa mujibu wa taratibu za chama.

Aidha, Dkt. Samia aliwataka wanachama wa CCM kujipanga kikamilifu kwa uchaguzi wa 2025 na kuepuka kubweteka, akiwahimiza kushiriki kikamilifu katika kampeni za chama na kutowabeza wapinzani.

Katika hotuba yake, pia aliwahimiza vijana na wananchi wote kuhakikisha wanajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kushiriki katika uchaguzi.

Akihitimisha, Dkt. Samia aliwashukuru wana-CCM kwa imani waliyoonesha kwake, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuwachagua kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, akisisitiza kuwa chama kitaendelea kuwa chaguo la wananchi kwa misingi yake ya haki na utumishi wa watu.

About the author

mzalendoeditor