Featured Kitaifa

MSIGWA ATAJA MIRADI ILIYOTEKELEZWA NA SERIKALI,IDADI YA WATALII YAONGEZEKA 

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ,Bw.Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro akielezea  utekelezaji wa Serikali wakati wa Mkutano uliofanyika leo Januari 25,2025 katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi,Morogoro.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ,Bw.Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro (hawapo pichani)  akielezea  utekelezaji wa Serikali wakati wa Mkutano uliofanyika leo Januari 25,2025 katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi,Morogoro.

 

Sehemu ya Waandishi wa habari pamoja na Watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wakimsikiliza  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ,Bw.Gerson Msigwa,(hayupo pichani)  akielezea  utekelezaji wa Serikali wakati wa Mkutano uliofanyika leo Januari 25,2025 katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi,Morogoro.

Na.Alex Sonna-MIKUMI MOROGORO

SERIKALI imetaja utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayoendelea kufanya na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kuendelea kuwaletea maendelea watanzania huku mapato yatokanayo na sekta ya utalii yakizidi kupaaa.
Hayo yameelezwa leo  Januari 25,2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ,Bw.Gerson Msigwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Serikali katika Hifadhi ya Taifa  Mikumi Mkoani Morogoro .
 ,Bw. Msigwa,amesema Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kusimamia shughuli za uhifadhi, ukusanyaji wa mapato, utangazaji wa utalii na fursa za uwekezaji ndani na nje ya nchi.
Amesema katika kuhakikisha dhamana hiyo inafikiwa, Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA) imeendelea kutekeleza mambo mbambali ikiwemo Kuhifadhi wanyamapori, bioanuai na makazi ya wanyama katikaHifadhi za Taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vya baadae.
Msigwa amesema  Shirika limeongeza matumizi ya sayansi na teknolojia katika uhifadhi hasa kwa viumbe adimu na vilivyo katika hatari ya kutoweka ili kuhakikisha ulinzi wao umeimarika na idadi inaongezeka.
Aidha amesema kuwa wameendelea kuboresha mahusiano na wananchi waishio jirani na Hifadhi kupitia mpango wa ujirani mwema kwa kutoa elimu ya uhifadhi, kutatua migogoro ya mipaka na kushirikiana nao katika maendeleo ya Uhifadhi, ujenzi wa miradi mbalimbali na uboreshaji wa huduma za kijamii.
Pia ameeleza kuwa wamefanikiwa  kulipa fidia kwa wakazi zaidi ya 3,500 wa kata ya Nyatwali iliyopo Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara ili eneo hilo liwe sehemu ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutokana na umuhimu wake katika ikolojia ya wanyamapori na shughuli za uhifadhi.
“Eneo hilo lina ukubwa wa ekari 14,250 na linafahamika kama “Ghuba ya Speke”.Kuimarisha ulinzi wa maliasili zilizo ndani ya Hifadhi za Taifa kwa kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama kwa kutumia teknolojia katika doria na ufuatiliaji wa mienendo ya wanyamapori adimu wakiwemo Faru, Sokwe na Mbwa mwitu ambao idadi yao inazidi kuongezeka,”amesema Msigwa
Uhifadhi na utalii katika hifadhi za taifa Tanzania.
Katika uhifadhi na utalii,Msigwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada kubwa za kutangaza utalii na fursa za uwekezaji nchini.
Amesema jitihada hizo zimezaa matunda kwani ameifungua nchi kiutalii na uwekezaji kupitia filamu aliyoiongoza ya “Tanzania: The Royal Tour” na baadae “The Amazing Tanzania”.
ONGEZEKO LA WATALII.
Msigwa amesema filamu hizo zimeleta matokeo chanya katika sekta ya utalii na kuchangia ongezeko kubwa la idadi ya watalii, sambamba na ongezeko la uwekezaji na mapato yatokanayo na utalii.
Pia, kumekuwa na ongezeko la safari za ndege za moja kwa moja kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kuja Tanzania kupitia mashirika kama KLM, Qatar Airways, Emirates na Turkish Airlines.
Amesema utalii kwenye Hifadhi za Taifa umeendelea kukua pia idadi ya watalii na mapato yameongezeka mwaka hadi mwakaa.
Msigwa amesema  Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2023/2024 watalii milioni 1,863,108 walitembelea hifadhi za Taifa.
Hata hivyo amesema kuwa watalii wameengezeka,Idadi hii imeongezeka ikilinganishwa na watalii milioni 1,618,538 waliotembelea Hifadhi za Taifa mwaka 2022/2023 ambalo ni ongezeko la watalii 244,570 sawa na asilimia 15.1.
Vilevile, kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Shirika lilikadiria kupokea watalii  milioni 1,848,759 ambapo kwa kipindi cha miezi sita Julai – Disemba 2024 watalii milioni 1,146,438 walitembelea Hifadhi za Taifa ambayo ni sawa na asilimia 62 ya makadirio ya mwaka.
Amesema ongezeko hilo la watalii limeenda sambamba na ongezeko la mapato ambapo kwa kipindi cha Julai – Juni 2023/2024, Serikali kupitia TANAPA lilipanga kukusanya shilingi bilioni 382,307,977,497.07 na limefanikiwa kukusanya Shilingi  bilioni 410,903,648,082.3 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.5 ya mapato yaliyokusudiwa kukusanywa kwa kipindi husika.
“Mapato hayo ni ongezeko la asilimia 21.8 ukilinganisha na 2022/2023 ambapo kiasi cha Shilingi 337,424,076,896.29 zilikusanywa,”amesema Msigwa
Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia TANAPA lilikadiria kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni  430,864,198,480, ambapo katika kipindi cha miezi sita Julai hadi Disemba 2024 Shirika limekusanya kiasi cha Shilingi bilioni 325,146,978,076.63 sawa na asilimia 75.5 ya malengo ya
makusanyo ya mwaka.
TUZO
Kuhusu Tuzo Bw. Msigwa amesema Tanzania imeendelea kung’ara kwa kupata tuzo  nyingi za Kimataifa.
Katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2024, Tanzania imeshinda na kupokea tuzo tatu (3) za kimataifa na tuzo moja (1) ya ndani ya nchi za kutambua umahiri na ubora katika kutoa huduma, uhifadhi na utalii na uandaaji wa taarifa za fedha.
Amesema tuzo hizo zinaakisi umahiri wa TANAPA katika uhifadhi na utoaji wa huduma bora
zinazoipa heshima Tanzania kimataifa.
Amesema  tuzo zilizotolewa ni pamoja na  ya umahiri na ubora wa huduma kwa wateja (Quality Choice Prize 2024) iliyotolewa tarehe 9 Disemba, 2024, Jijini Vienna, Austria na Shirika la European Society for Quality Research (ESQR).
“Hii ni Tuzo ya tano (5) mfululizo ambayo Shirika letu limekua likishinda kotokana na utoaji wa
huduma bora kwa wateja kwa viwango vya kimataifa,” amesema Msigwa
Ameitaja tuzo nyingine ni ya  Hifadhi Bora Afrika (Africa’s Leading National Park 2024)
“Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa mara ya sita (6) mfululizo imefanikiwa kuwa Hifadhi Bora Afrika (Africa’s Leading National Park 2024) na kupewa tuzo hiyo Jijini Mombasa, Kenya na Shirika la “World Travel Awards”,”amesema Msigwa
MIUNDOMBINU HIFADHINI
Msigwa amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara za utalii (tourist circuits), viwanja vya ndege, malango ya kukusanyia fedha na huduma za malazi ili kuvutia watalii zaidi kutembelea Hifadhi na kuongeza mapato.
Amesema  lengo la kuboresha huduma kwa wageni ni kutokana na juhudi zilizofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio vilivyoko nchini kupitia filamu ya Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania.
Amesema Serikali imeanza mchakato wa kujenga barabara kuu zinazotumika zaidi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa kiwango cha tabakagumu ili kupunguza athari za mazingira, kuboresha huduma kwa
watalii na kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara.
Pia Serikali imewekeza kwenye teknolojia ya kisasa ya matumizi ya ‘smart gates’ na ufungaji wa ‘CCTV cameras’ kwenye baadhi ya malango ya kuingilia, kutokea wageni na maeneo mengine muhimu.
Vilevile kuboresha ukusanyaji wa mapato, kuhakikisha usalama wa watalii na kurahisisha utoaji wa huduma.
“Kukarabati viwanja vya ndege 11 katika maeneo ya barabara za kuruka na kutua ndege (runway) zinazobeba watalii pamoja na Maendeleo ya shirika letu la reli Tanzania (TRC),”amesema Msigwa
TRC
Bw.Msigwa  amesema  Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa TRC katika kutekeleza Majukumu yake, mpaka sasa inafurahisha kwamba ndani ya miezi mitano ya huduma za SGR, zaidi ya abiria 1,500,000
wameshasafiri na reli hiyo huku mapato mpaka kufikia mwisho wa mwezi Desemba 2024 yakifikia shilingi Bilioni 37.6.
“Mkakati tunaokwenda nao sasa ni reli yetu ya SGR kuanza kusafirisha mizigo kwa vipande vya Dar es Salaam hadi Dodoma kiasi cha tani milioni 1 kwa mwaka, lengo ni kukuza ushoroba wa kibiashara na kimaendeleo unaochochea uzalishaji na ajira kwa wananchi kote inapopita.
Vile vile, amesema wanaendelea kukamilisha  kipande cha Mwanza hadi Isaka na kukifanya kianze kutoa
huduma.
“Ujenzi wa vipande vyengine hadi Kigoma vitaendelea kujengwa kama ilivyopangwa,”amesema Msigwa
MWENENDO WA UKUSANYAJI WA MAPATO NCHINI
Msigwa amesema Tanzania imeendelea kushuhudia kuimarika na kukua kwa shughuli za kiuchumi zilizochangia kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.
” Hali hii imetokana na uongozi shupavu wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ambaye amekua mstari wa mbele katika kusimamia na kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali ambayo yameiwezesha nchi kuwa imara,”amesema
SEKTA YA MAWASILIANO 
Bw.Msigwa   amesema sekta ya Mawasiliano nchini inajumuisha sekta ndogo ya Simu na Intaneti,
Utangazaji, na Posta na Usafirishaji wa vifurushi na vipeto.
Amesema kwa kipindi cha miaka minne (4) ya Serikali ya awamu ya sita (6) chini ya uongozi wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Sekta ya mawasiliano imekua na kuwezesha sekta nyingine za kiuchumi na wananchi kwa ujumla kuwezeshwa kijamii na kiuchumi.
HUDUMA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA).
Amesema mpaka kufikia Disemba mwaka huu, vitambulisho vya Taifa (NIDA) imechapisha na kusambaza vitambulisho milioni 21,115,671.
Amesema Kati ya vitambulisho hivyo, vitambulisho milioni 20,082,768 vilichukuliwa na wananchi husika na zaidi ya Vitambulisho 1,000,000 vilikuwa havikuchukuliwa na wananchi vikaendelea kukaa kwenye ofisi za Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji.
Amesema NIDA imeamua kukusanya vitambulisho vyote na kuvirudisha katika
ofisi za NIDA za Wilaya,
Pia NIDA kwa kushirikiana na TCRA inatuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi (sms) kwa wale wote waliokuwa hawajachukua vitambulisho vyao kwenda kuvichukua ndani ya mwezi mmoja tangu kupata sms vinginevyo matumizi ya Namba yatasitishwa.
SEKTA YA UMEME 
Msigwa amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji wa umeme mijini na vijijini ili kufikia lengo la Dunia la wananchi wote kuwa wamefikiwa na nishati ya umeme na kufanya hali ya huduma za umeme nchini kuimarika.
Amesema kuwa uzalishaji wa umeme sasa umefikia jumla ya Megawati 3,169 ikilinganishwa na mahitaji ya megawati 1,888.
“Wananchi waliofikiwa na huduma ya umeme ni asilimia 78.4 ( Mijini asilimia 99 na 69.6), kasi ya  kuunganisha umeme imeendelea kuongezea ambapo hadi kufikia mwezi Desemba, 2024 vjijiji 12,318 vimeunganishwa na umeme kutoka vijiji 8247 mwaka 2021.”amesema
SEKTA YA MICHEZO
Amesema kuwa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu limetaja Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuwa ligi ya nne bora barani Afrika kwa kushika nafasi ya 57 duniani kwa mwaka 2024.
“Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo inaendelea na uratibu wa ujenzi na ukarabati wa viwanja kwa ajili ya mashindano na mazoezi ya CHAN 2024 na AFCON 2027.”amesema Msigwa
Hata hivyo amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa viwanja mbalimbali vya  Mpira wa miguu uwanja wa Samia Stadium unaojengwa  jiji la Arusha ambao utatumika katika Michuano ya AFCON 2027 pamoja viwanja vya Michezo vilivyopo mkoani Dodoma.

About the author

mzalendoeditor