Featured Kitaifa

KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA HAKI KWA WANANCHI

Written by mzalendoeditor

Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imezinduliwa rasmi mkoani Mtwara, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

 

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo katika uwanja wa Nangwanda, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, na kuhudhuriwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala.

Katika hotuba yake, Kanali Sawala amewataka wananchi wa Mtwara kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma za kisheria zitakazotolewa bure, huku akisisitiza kuwa hii ni fursa muhimu kwa kila mmoja kushiriki katika kutatua migogoro ya kisheria.

Kanali Sawala ameeleza kuwa kampeni hii itasaidia kuongeza uelewa kuhusu haki za binadamu, hasa haki za wanawake na watoto, na itajikita zaidi katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwa ni pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia na haki za familia.

Lengo kuu la kampeni ni kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, kuongeza uelewa wa haki za binadamu, na kutoa msaada wa kisheria kwa jamii, wakiwemo manusura wa ukatili wa kijinsia. Aidha, kampeni hii inatarajiwa kuelimisha umma kuhusu sheria na masuala ya utawala bora, ambayo yatasaidia kuongeza amani na utulivu mkoani Mtwara.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kwa Umma kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Abdulrhaman Mshamu, amesema kuwa kampeni hii mkoani Mtwara itadumu kwa siku kumi na kuwa ni sehemu ya mfululizo wa kampeni zilizofanyika katika mikoa mingine 11 tangu mwaka 2023, na mikoa sita inayoendesha kampeni hiyo nchini.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Rose Ebrahim, amesisitiza kuwa Mahakama inashirikiana kikamilifu na serikali katika kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wananchi kwa wakati, na kuwa kampeni hii ni muhimu katika kufanikisha malengo ya haki ya mwananchi.

Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wameelezea furaha yao kwa kupewa huduma ya kisheria kwa urahisi, wakiamini kuwa kampeni hii itasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria walizokuwa wakikabiliana nazo kwa muda mrefu.

About the author

mzalendoeditor