Featured Kitaifa

HAKIKISHENI UANDIKISHAJI WA WATOTO WENYE UMRI WA KUANZA ELIMU YA AWALI NA DARASA LA KWANZA UNAKAMILIKA KWA WAKATI

Written by mzalendoeditor

Na. OR – TAMSIEMI, Muleba Kagera

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia elimu ya Msingi Bi. Susan Nussu amewataka Maafisa Elimu Kata na Walimu Wakuu kote nchini, kila mmoja ahakikishe uandikishaji wa watoto wote wenye umri wa kuanza Elimu ya Awali na Darasa la Kwanza unafanyika na kukamilika mapema ili kuwapa fursa walimu kuendelea kufundisha.

Bi. Nussu amesema hayo tarehe 20/1/2025 kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -TAMISEMI Bw. Adolf Nduguru wakati akifunga Mafunzo ya Walimu wa Elimu ya Awali Na Walimu Wakuu katika Chuo cha Ualimu Katoke, Kagera.

Amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 inasisitiza utoaji wa elimu bora, kuanzia Elimu ya Awali ambayo ndiyo msingi wa kwanza katika mfumo wa Elimu rasmi kote ulimwenguni. Pia amesema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa Elimu ya Awali ina mchango mkubwa katika makuzi na malezi ya mtoto kiakili, kimwili na kijamii.

‘Programu ya BOOST inayotekelezwa na WyEST kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imelenga katika kuwekeza kwa watoto wa Elimu ya Awali kwa kuandaa Kitita cha Ubora cha Kujifunza katika Elimu ya Awali ili kuimarisha ujifunzaji wa watoto wa Elimu ya Awali kulingana na hatua za makuzi” amesema Nussu

Aidha, amesema, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa elimu bila ada kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Sita kwa kuongeza fedha za kugharamia mpango huo kutoka shilingi bilioni 249.7 mwaka 2020/21 hadi shilingi bilioni 484.3 mwaka 2024. Jumla ya shilingi trilioni 1.304 zimetolewa kati ya mwaka 2020/21 hadi Desemba 2024.

“Idadi ya wanafunzi wanaonufaika imeongezeka kutoka 13,888,694 mwaka 2020/21 hadi 15,298,054 mwaka 2024”

Ameongezea kwa kutoa wito kwa wazazi wote wenye wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari wahimizwe kuwapeleka shule wanafunzi hao mepama iwezekanavyo ili kuepuka kukosa mafunzo kabilishi (orientation course) yanayotolewa kama msingi wa ujifunzaji katika ngazi hiyo ya elimu.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndugu. Isaya Mbenja amesema anaenda kusimamia utekelezaji wa mafunzo yote yaliyotolewa kwa walimu hao kwa vitendo kwa kuzingatia mahitaji maalumu ili kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu nchini.

Mafunzo hayo yalitolewa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu yamenufaisha walimu katika halmashauri zote 184 kwa kufundishwa mada mbalimbali zikiwemo nyenzo za kufundishia jumla ya walimu 3,000 wa elimu ya awali ambapo jumla ya washiriki 18,564 wamejengewe uwezo wakiwemo walimu wa elimu ya awali 9670, wakuu wa shule 9,302 kutoka shule 9,302, maafisa elimu wa mikoa 26, wakuu wa divisheni ya elimu msingi 184.

About the author

mzalendoeditor