Featured Kitaifa

WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI LINDI, MTWARA, RUVUMA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA NA KANUNI

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari akizungumza hii leo Januari 18, 2025 wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ngazi ya mkoa, mkoani Lindi ambapo amewataka watendaji hao  kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, maelekezo na miongozo itakayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.  Dkt. Zakia Mohamed Abubakar akizungumza hii leo Januari 18, 2025 wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ngazi ya mkoa, mkoani Mtwara ambapo amewahimiza watendaji hao kuhakikisha wanahamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao.

 

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira akizungumza hii leo Januari 18, 2025 wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ngazi ya mkoa, mkoani Ruvuma kwa Watendaji wa Halmashauri za Madaba, Namtumbo na Tunduru ambapo amewataka kuwa makini katika kila eneo la usambazaji na utunzaji wa vifaa, mafunzo yote na muda sahihi wa ufunguaji na ufungaji wa vituo vya kuandikishia wapiga kura.
*******************
Na. Mwandishi Wetu
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma wametakiwa kutekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, maelekezo na miongozo itakayotolewa
na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
 
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Tume ambaye
pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omar leo tarehe 18 Januari, 2025 wakati
akifunga mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari ngazi ya mkoa, Mkoani Lindi
ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
 
“mnapaswa kutekeleza majukumu mliyopewa kwa
kuzingatia sheria, kanuni, maelekezo na miongozo itakayotolewa na Tume,”
amesema Jaji Asina.
 
Amewaasa watendaji hao kutambua uzito na
umuhimu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari na kwamba elimu na ujuzi walioupata
vitawasaidia kutekeleza kwa nadharia na vitendo yale yote waliyofundishwa.
 
“Mnapaswa kutambua uzito na umuhimu wa zoezi
hili la kitaifa na kwamba baada ya ninyi kufundishwa na kuelekezwa ipasavyo
katika mafunzo haya, elimu na ujuzi mliopata vitawasaidia kutekeleza kwa
nadharia na vitendo yale yote mliyofundishwa,” amesema.
 
Akifunga mafunzo kama hayo mkaoni Mtwara,
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.
Dkt. Zakia Mohamed Abubakar amewahimiza watendaji hao kuhakikisha wanahamasisha
wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba
itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao.
 
“Ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya
zoezi hili kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura
halali.
 
 Jukumu
la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja ninyi watendaji, kwa kushirikiana na
wadau wengine katika maeneo yenu kupitia nyenzo mlizo nazo,” amesema Mhe.
Zakia.
 
Mkoani Ruvuma mafunzo hayo yamefungwa na
Mjumbe wa Tume, Mhe. Magdalena Rwebangira ambaye aliwakumbusha watendaji hao
kuwa makini katika kila eneo la usambazaji na utunzaji wa vifaa, mafunzo yote
na muda sahihi wa ufunguaji na ufungaji wa vituo vya kuandikishia wapiga kura.
 

Mafunzo hayo yamefanyika
ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari mkoani Mtwara, Lindi na mkoa wa Ruvuma
kwenye Halmashauri za Wilaya ya Madaba, Namtumbo na Tunduri  ambapo uboreshaji utafanyika kwa siku saba
kuanzia tarehe 28 Januari, 2025 hadi tarehe 03 Februari, 2025 na vituo
vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

 

Mwenyekiti wa Mafunzo Mkoani Mtwara, Ndg. George Mbogo akizungumza.

 

 
Meza kuu Mkoani Lindi 

 

Watendaji mkoani Mtwara wakifuatilia hotuba ya kufunga mafunzo.

 

Mafunzo kwa vitendo mkoani Mtwara

 

 

Watendaji Mkoani Ruvuma wakimsikiliza mgeni rasmi akifunga mafunzo hayo. 

 

Watendaji Mkoani Lindi wakimsikiliza mgeni rasmi akifunga mafunzo hayo. 

 

 

Watendaji Mkoani Lindi wakifanya mafunzo kwa vitendo.


About the author

mzalendo