Featured Kitaifa

NCC YAHIMIZA UJENZI WA MAJENGO SALAMA NA YANAYOZINGATIA AFYA YA WATUMIAJI

Written by mzalendoeditor

Timu ya wahandisi kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi(NCC) wakifanya mapitio ya rasimu ya kanuni za majenzi (Building Codes) na maoni yaliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu kanuni hizo. 

Na.Mwandishi Wetu-Morogoro

Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) linaendesha zoezi la kufanya mapitio ya rasimu ya kanuni za majenzi (Building Codes) na maoni yaliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu kanuni hizo. Zoezi hili la wiki mbili linaongozwa na timu ya wahandisi chini ya usimamizi wa Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Mhandisi Matiko Mturi (PhD).

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhandisi Geofrey Mwakasenga ameeleza kuwa NCC lina jukumu la kuandaa, kuratibu, na kusimamia maendeleo ya viwango, kanuni, na miongozo ya sekta ya ujenzi nchini. “Kanuni hii itakuwa moja ya misingi ya sheria ya ujenzi ambayo pia Baraza linasimamia,” amesema Mhandisi Mwakasenga.

Kanuni hizo zinatarajiwa kuwa muongozo wa kitaifa wa kusimamia usalama wa majengo, usalama wa watumiaji, na kuhakikisha majengo yanazingatia utunzaji bora wa mazingira, ndani na nje ya jengo.

Aidha, Mhandisi Mwakasenga ametoa wito kwa wadau wa sekta ya ujenzi kutumia kanuni hizo mara zitakapokamilika, akibainisha kuwa zitaleta manufaa makubwa kwa kupunguza athari zinazotokana na ujenzi usiozingatia viwango.

 “Tunaomba wadau wote wa tasnia ya ujenzi kutumia kanuni hizi mara zitakapokamilika ili kupunguza au kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika ujenzi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Msanifu Majengo Arch. Mariahildergard Byarufu amesema kuwa kanuni hizi zitasaidia kuimarisha viwango vya ujenzi na kuhakikisha mazingira rafiki kwa watumiaji wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum. “Kupitia kanuni hizi, majengo yatakuwa na nafasi zinazokidhi viwango vinavyotakiwa, na kuwezesha kundi hili kutumia majengo bila kuhitaji msaada wowote,” amesema Arch. Byarufu.

Kwa sasa, NCC inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kanuni hizo zinakamilika kwa wakati na kuleta mageuzi chanya katika sekta ya ujenzi nchini. 

About the author

mzalendoeditor