Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.George Simbachawene, akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 11,2024 jijini Dodoma kuhusu usaili unaotarajiwa kufanyika kuanzia Januari 14 hadi Februar 24, mwaka huu kwa walimu 201,707.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.George Simbachawene, akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 11,2024 jijini Dodoma kuhusu usaili unaotarajiwa kufanyika kuanzia Januari 14 hadi Februar 24, mwaka huu kwa walimu 201,707.
Na.Alex Sonna- DODOMA
SERIKALI imesema Jumla ya Walimu 201,707 wanatarajiwa kufanyiwa usaili kuanzia Januari 14 hadi Februar 24, mwaka huu kwa ajili ya kujaza nafasi 14,648 zilizo tangazwa na serikali, ili kupunguza uhaba wa walimu nchini.
Hayo yameelezwa leo Januari 11,2024 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usaili huo.
“Kuanzia tarehe 14 Januari hadi terehe 24 Februari, 2025, usaili wa kada za Ualimu utaendeshwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (UTUMISHI),“Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Tume ya Utumishi wa Walimu, Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma.”amesema
Waziri Simbachawene, amesema usaili huo una lengo la kujaza nafasi 14,648, zilizotolewa na Rais kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini.
Hata hivyo ameongeza kuwa kulingana na mahitaji yetu ya elimu kwa sasa, tutaajiri wataalamu wa fani za Amali. Hivyo, nawasihi sana wale wote watakaopata nafasi ya kuajiriwa, wawe tayari kujiendeleza ili kuweza kukidhi matakwa ya ajira zao katika Utumishi wa Umma.
Aidha, amesema usaili huo wa kada za ualimu utafanyika katika Mkoa ambao kila msailiwa anaishi lengo ni kuwapunguzia gharama za kusafiri na mambo mengine.
“Sekretarieti ya Ajira ilitoa matangazo kumtaka kila msailiwa kuhuisha taarifa zake katika akaunti yake ya Ajira Portal sehemu iliyoandikwa ‘current physical adress’ kwani ndipo tumewapangia vituo vya usaili kulingana na anuani walizojaza,”amesisitiza
Pia amewataka waombaji wote kuhakikisha kila mmoja anakwenda katika kituo ambacho amepangiwa kwa ajili ya usaili kwani mahitaji yake ya msingi yapo huko.
“Ninapenda kuwakumbusha wale wote watakaokwenda kwenye usaili wahakikishe wanabeba vyeti vyao halisi kikiwemo cheti cha taaluma na cheti cha kuzaliwa,”amesema
Hata hivyo amesisitiza kuwa usaili wa awali wa kuandika (Mchujo) kwa kada za Ualimu utafanyika kwa njia ya kuandika kwa mkono kwa kada zote na ngazi zote za elimu.