Featured Kitaifa

WAZIRI DKT. GWAJIMA APONGEZA HATUA NZURI ZA UJENZI WA MIRADI YA ELIMU KALIUA-TABORA

Written by mzalendoeditor

Na WMJJWM – TABORA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa hatua nzuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya elimu wilayani Kaliua.

Dkt. Gwajima alitoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Ulyankulu katika ziara yake ya kikazi mkoani Tabora Januari 9, 2025, mara baada ya kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye ujenzi wa miradi ya elimu ikiwemo miradi ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Langoni yenye thamani ya Shilingi milioni 361.5 kupitia Programu ya BOOST unakihusisha ujenzi wa madarasa tisa (9) na matundu kumi (10) ya choo.

Aidha, aliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa mabweni manne (4) ya wasichana na matundu kumi (10) ya vyoo katika Shule ya Sekondari Mkindo, mradi ambao umegharimu Shilingi milioni 136.

“Naomba kutumia fursa hii kuipongeza Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa kusimamia ipasavyo miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu. Nimekagua na kujionea hatua kubwa zilizofikiwa, na kilichonifurahisha zaidi ni kuona fedha shilingi bilioni 186.56 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya elimu mkoani Tabora zinatumika vizuri. Nawapongeza sana,” amesema Dkt. Gwajima.

Pia, Waziri Gwajima aliwahimiza wananchi wa Ulyankulu kuchangamkia fursa za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara ndogondogo kujisajili na kupata vitambulisho vya kidijitali vitakavyowawezesha kunufaika na mikopo kupitia Benki ya NMB

Aidha Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi na kuhakikisha malezi bora na kulinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Matiko Chacha, ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo ya elimu kutasaidia kuondoa changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule. Pia amesisitiza umuhimu wa wazazi kuhakikisha watoto wa umri wa shule wanapata elimu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Dkt. Gerald Mongela, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kujenga miundombinu ya elimu. Amebainisha kuwa kupitia miradi hiyo, wanafunzi vijijini sasa wanasoma bila changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Wilaya ya Kaliua ni miongoni mwa wanufaika wa juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya elimu, hatua inayolenga kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa wote.

About the author

mzalendoeditor