Featured Michezo

MHANDISI JUMBE APELEKA MASHABIKI WA STAND UNITED GEITA, ZAWADI NONO WAKISHINDA

Written by mzalendoeditor
Mratibu wa safari ya mashabiki wa Stand United FC kutoka Shinyanga kwenda Geita ,Jackline Isaro akizungumza na waandishi wa habari
 
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Mhandisi James Jumbe Wiswa, mdau mkubwa wa michezo, ameonyesha utayari wa kutunisha msukumo kwa timu ya Stand United FC na mashabiki wake, kwa kudhamini safari ya mashabiki wa timu hiyo kutoka mkoani Shinyanga kwenda mkoani Geita.

Safari hii imeandaliwa kwa ajili ya kushuhudia mechi muhimu ya Ligi ya Championship kati ya Stand United FC na Geita Gold FC, itakayochezwa Jumapili, Januari 12, 2025, majira ya saa 10 jioni, katika uwanja wa Nyankumbu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Januari 10, 2025, mkoani Shinyanga, Mratibu wa safari ya mashabiki wa Stand United FC ,Jackline Isaro,  amesema safari hiyo imedhaminiwa na Mhandisi James Jumbe Wiswa kama sehemu ya juhudi za kuendeleza michezo mkoani Shinyanga na kuimarisha heshima ya timu ya Stand United FC ‘Chama la Wana’.

Jackline Isaro 

Jackline amefafanua kuwa Mhandisi Jumbe, ambaye ni mkazi wa Shinyanga na pia ni mpenzi mkubwa wa michezo, ameonyesha dhamira ya dhati kwa kuhamasisha mashabiki wa timu hiyo kwenda kushangilia timu yao huko Geita. 

Aidha, Jackline amesema pia Mhandisi James Jumbe ametangaza zawadi ya shilingi milioni tatu kwa timu ya Stand United FC endapo itashinda mchezo huo dhidi ya Geita Gold FC na kwamba ataendelea kutoa motisha kwa kila goli litakalofungwa na Stand United, kwa kutoa shilingi 200,000 kwa kila goli.

“Mhandisi James Jumbe Wiswa ameichukulia kwa uzito mechi hii kati ya Stand United FC na Geita Gold FC, kwa kuwa yeye ni mkazi wa Shinyanga pia ni mwanamichezo amewaahidi mashabiki wa Stand United FC kwamba safari yao itakuwa na mafanikio na kwamba endapo timu itashinda na kupata pointi tatu, atatoa zawadi ya shilingi milioni tatu. Pia motisha ya shilingi 200,000/= ambayo ameendelea kutoa kwa kila goli litakalofungwa na timu ipo pale pale,” amesema Jackline.

Mhandisi James Jumbe Wiswa

Jackline ameongeza kuwa safari hii ni sehemu ya juhudi za kurudisha heshima ya soka mkoani Shinyanga, huku akiwahimiza wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao, Stand United FC. 

“Tunataka kurudisha heshima ya mkoa wa Shinyanga kwa kuiinua timu hii inayodhaminiwa na Jambo Group. Tunaendelea kuunga mkono na juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo nchini,” amesisitiza Jackline.

Kwa upande mwingine, Jackline amethibitisha kuwa zaidi ya mashabiki 200 wanatarajiwa kuondoka kwenda Geita kwa ajili ya mchezo huo na kwamba tayari Mhandisi Jumbe ameshalipia usafiri wa magari kwa ajili ya safari ya mashabiki.

Pia, amebainisha kwamba Mhandisi Jumbe ameendelea kusaidia timu ya Stand United FC katika kuimarisha kikosi chao, ambapo ameisaidia timu hiyo kusajili wachezaji wawili wapya.

Afisa Habari wa Stand United FC, Ramadhani Zoro, ametoa shukrani za dhati kwa Mhandisi Jumbe kwa msaada wake mkubwa kwa timu. 

Ramadhani Zoro

Amesema motisha hii itachangia katika kushinda mchezo dhidi ya Geita Gold FC. 

“Tunamshukuru Mhandisi Jumbe kwa motisha hii. Kusafirisha mashabiki zaidi ya 200 kwenda mkoani Geita si jambo dogo. Nasi tunaahidi kurudi na ushindi, tumejiandaa vyema kwa mchezo huu na kikosi  tayari kimeelekea Geita,” amesema Zoro.

Kwa upande wao mashabiki wa Stand United FC wamemshukuru Mhandisi Jumbe kwa kuonyesha upendo na dhati kwa timu hiyo wakisema misaada yake inawafanya waamini kuwa soka la Shinyanga linaheshimiwa na limejengwa kwa nguvu za pamoja.
“Mhandisi Jumbe, wewe ni mchezaji wa pili kwenye timu yetu! Ahsante kwa kutufanya tuwe na matumaini ya ushindi. Umetusaidia kwa njia nyingi, na safari hii kwenda Geita tutashinda. 
Asante kwa kuwa kiongozi wa kweli na mdau wa michezo, tutaipigania Stand United kwa nguvu zote!”,wamesema
“Mhandisi Jumbe, tunakushukuru sana kwa kusaidia timu yetu na kututia moyo. Msaada wako umejenga matumaini mapya na utatufanya tuendelee kupigania nafasi yetu kwenye Ligi Kuu. Wewe ni mfano wa kweli wa mdau wa michezo na tunajivunia kuwa na watu kama wewe kwenye jamii yetu. Safari yetu kwenda Geita itakuwa na mafanikio, na tutaleta ushindi!”,wameongeza.

Mchezo huu ni muhimu kwa timu zote mbili, kwani Stand United FC ipo nafasi ya nne kwenye ligi hiyo, huku Geita Gold FC ikiwa nafasi ya tatu. 

Timu zote zinapigania kupanda Ligi Kuu ya Tanzania Bara, na ushindi huu unaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika mchakato wa kupanda daraja.
Mratibu wa safari ya mashabiki wa Stand United FC kutoka Shinyanga kwenda Geita ,Jackline Isaro akizungumza na waandishi wa habari
Mratibu wa safari ya mashabiki wa Stand United FC kutoka Shinyanga kwenda Geita ,Jackline Isaro akizungumza na waandishi wa habari
Afisa Habari wa Stand United FC, Ramadhani Zoro akizungumza na waandishi wa habari
Mhandisi James Jumbe Wiswa

About the author

mzalendoeditor