Featured Kitaifa

DKT. NCHEMBA ATETA NA BALOZI WA KOREA NCHINI

Written by mzalendoeditor
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (Kulia), akiagana na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Eunju Ahn, baada ya kikao chao jijini Dodoma, ambapo walijadiliana mambo mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo, kikao kilichohudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (Katikati) akizungumza jambo wakati wa kikao chake na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Eunju Ahn (hayupo pichani) jijini Dodoma, ambapo walijadiliana mambo mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi ikiwemo ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban (watatu kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi, Bw. Juma Mkabakuli (wa tatu kulia) Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Patrick Pima (wa pili kushoto), na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (Kulia), akimkabidhi zawadi ya baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini, Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Eunju Ahn, baada ya kikao chao jijini Dodoma, ambapo walijadiliana mambo mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi ikiwemo ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kikao kilichohudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (wa sita kushoto) na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Eunju Ahn (wa tano kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban (wa sita kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi, Bw. Juma Mkabakuli (wa tano kulia), Msaidizi wa Balozi wa Korea, Bw. Sugnyun Lee (wa nne kushoto), Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Patrick Pima (wa nne kulia), na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kumalizika kwa kikao chao, jijini Dodoma, ambapo walijadiliana mambo mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo.
 (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa dola za Marekani bilioni 2.5 zilizoahidiwa kutolewa na Jamhuri ya Korea Kusini kwa Tanzania hivi karibuni, zitasaidia kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo itakayochangia kusisimua ukuaji wa uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania kwa ujumla.
 
Dkt. Nchemba amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mhe. Eunju Ahn, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili.
 
“Nchi yetu inasubiri kwa hamu kubwa utekelezaji wa miradi inayotokana na fedha hizo na hata katika Hotuba yake ya Mwisho wa Mwaka 2024, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alielezea kwa kina namna fedha hizo zitakavyotumika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kutimiza ajenda ya kitaifa ya kuwaletea watanzania Maendeleo” Alisema Dkt. Nchemba.
 
Alieleza kuwa makubaliano ya miradi itakayotumia fedha hizo iko katika sekta muhimu za maendeleo itakayochangia kukuza ajira, uchumi na maendeleo ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
 
Dkt. Nchemba aliahidi kuwa Tanzania iko tayari kuongeza kasi ya ushirikiano kati ya nchi hizo ili kufanikisha malengo ya uhusiano uliodumu kwa miaka mingi kati yake na Korea kwa faida ya wananchi wa pande hizo mbili.
 
Kwa upande wake, Balozi wa Korea Kusini hapa nchini, Mhe. Eunje Ahn, alisema kuwa Korea inaitazama Tanzania kama mdau wake mkubwa wa maendeleo ambapo haijawahi kushuhudiwa nchi yoyote Barani Afrika ikipewa fedha nyingi kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5, kwa wakati mmoja kama ilivyofanyika kwa Tanzania.
 
Mhe. Ahn aliseza kuwa kupitia fedha hizo, Korea itaisaidia Tanzania kutekeleza miradi 12 ya kimkakati iliyowasilishwa na Serikali, ambayo inatarajiwa kukuza uchumi wa nchi kupitia miradi mbalimbali itakayotekelezwa na Serikali pamoja na Sekta Binafsi.
 
Alisema kuwa Korea inaiona Tanzania kuwa nchi yenye maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii na kwamba muda mfupi ujao itafikia viwango vya juu vya ukuaji wa Uchumi kutokana na umahili wa usimamizi wa shughuli zake za kiuchumi ikilinganishwa na mataifa mengi ya kiafrika na ulimwengini kwa ujumla
 
Katika kikao chao, Mhe. Dkt. Nchemba na Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mhe. Eunje Ahn, walijadiliana kuhusu fedha, dola bilioni 2.5 ambazo mkataba wake ulisainiwa tarehe 2 Juni, 2024 nchini Korea na kushuhudiwa na Marais wa nchi hizo mbili pamoja na kuondoa changamoto ya utozaji kodi mara mbili na ukwepaji kodi kwa kampuni zinazowekeza katika nchi hizo mbili pamoja na kuvutia uwekezaji.

About the author

mzalendoeditor