Na. Lusungu Helela – Mpwapwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe.George Simbachawene ametoa wito kwa Watanzania wenye sifa za kujiandikisha katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza kwa wingi katika vituo ili kupata Kitambulisho cha Mpiga Kura kitakachowawezesha kupata haki ya kuchagua Viongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao .
Pia, Mhe.Simbachawene amewataka Watumishi wa Umma nchini kuhakikisha wanatumia haki yao kujiandikisha kwenye daftari hilo ili kuwawezesha kuchagua viongozi akiwemo Rais, Wabunge pamoja na Madiwani kwenye uchaguzi huo .
Mhe.Simbachawene ametoa wito huo leo Jumatatu Desemba 30, 2024 mara baada ya kuboresha taarifa zake kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo cha Wapiga Kura kilichopo Kata ya Pwaga Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Amesema kitendo cha kwenda kuboresha taarifa katika kituo husika kwa Mtumishi wa Umma ni kujihakikishia usahihi wa taarifa zake pamoja na uhakika wa mahali atakapopigia kura.
“ Nimefika hapa ndani ya muda mfupi nimeboresha taarifa zangu ambapo nimepata kitambulisho kipya kitakachoniwezesha kutumia haki yangu ya kidemokrasia muda utakapowadia wa
kuchagua na kuchaguliwa ”, amesema Mhe.Simbachawene.
Katika hatua nyingine Mhe.Simbachawene ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuboresha zoezi hilo na kufanya kazi kwa weledi inayoimarisha Demokrasia nchini huku akisifu jinsi zoezi hilo linavyoendesha kwa umakini na uharaka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zingine za kujiingizia kipato
Aidha, Mhe.Simbachawene amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuendelea kuimarisha Demokrasia nchini na kuendelea kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Awali, Mwandikishaji wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo hicho Bi. Christina Chigohe ameeleza kuwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linafanyika kwa siku saba ambapo lilianza Desemba 27 na litafikia tamati Januari 3, 2025.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea unaongozwa na kaulimbiu “Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora”