Featured Kitaifa

WAZIRI SIMBACHAWENE AZINDUA MAADHIMISHO YA WIKI YA MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU

Written by mzalendoeditor

Waziri  wa  Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akizindua  Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa kwa mwaka 2024.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imezindua Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa kwa mwaka 2024, kilele chake kitafanyika Disemba 10,mwaka huu ambayo itatumika  katika kufanya tathmini na utatuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria kwa wahitaji hasa kwenye magereza na masuala ya utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa nchini. 

Akizindua madhimisho hayo leo Disemba 5,2024 jijini Dodoma Waziri  wa  Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene,amesema mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika tofauti kidogo.

“Kwa muda wa miaka miwili mfululizo maadhimisho haya yamefanyika kwa mtindo wa wiki ya huduma kwa umma ambapo wananchi walipata fursa ya kukutana ana kwa ana na watoa huduma na kupata huduma katika viwanja vya Nyerere Square hapa jijini Dodoma.”amesema Waziri Simbachawene

Aidha ameongeza kuwa mwaka huu wa 2024, maadhimisho haya yatafanyika tofauti kidogo ambapo Watumishi wa Umma watafanya kongamano kujitathmini kuhusu uzingatiaji wa haki za binadamu na kuepuka rushwa wanapotoa huduma kwa umma.

“Lengo  la Kongamano hilo ni kuwapa fursa watoa huduma ambao ni Watumishi wa Umma kujitathmini ni kwa namna gani wanatekeleza jukumu la Serikali la Ustawi wa Wananchi kwa kuzingatia Haki za Binadamu na kuepuka vitendo vya rushwa na  namna wanavyowajibika kwa Umma.”amesema

Hata hivyo ameeleza kuwa katika Kongamano hilo, zitawasilishwa na kujadiliwa mada mbili ambazo ni “Haki za Binadamu katika Mapambano Dhidi ya Rushwa” na “Maadili, Haki na Wajibu wa Watumishi wa Umma.”. 

Katika hatua nyingine Simbachawene,amesema  katika maadimisho ya mwaka huu taasisi zinazosimamia  utawala bora zitafanya ziara katika magereza ya Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma na kuwasikiliza wafungwa na mahabusu na kutoa misaada ya kijamii.

Waziri Simbachawene amesema kupitia vyombo mbalimbali vya habari zikiwemo redio, runinga na mitandao ya kijamii, viongozi na watumishi wa taasisi zinazoratibu maadhimisho haya watatoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yahusuyo Maadili, Haki za Binadamu na juhudi dhidi ya Rushwa.

Pia Waziri Simbachawene amezitaja taasisi zinazoshirikiana katika kuadhimisha Siku hiyo  ni pamoja na Ofisi ya Rais, Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Katiba na Sheria, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani.

“Maadhimisho hayo yatafanyika katika ngazi za Kanda kwa kushirikisha taasisi hizo kwa maeneo yale ambapo Taasisi nilizozitaja hapo juu zina ofisi.”amesema

 

About the author

mzalendoeditor