Featured Kitaifa

UDOM YAANZA KUTENGENEZA SERA NA MIONGOZO MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA AKILI MNEMBA

Written by mzalendoeditor

 

MAKAMU Mkuu wa Chuo  Kikuu cha Dodoma (UDOM) Prof. Lugano Kusiluka,akizungumza wa kongamano la 15 la Wahitimu wa Chuo hicho,hafla iliyoanza leo Disemba 4 hadi Disemba 6,2024 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki wakisikiliza mada mbalimbali wakati wa  kongamano la 15 la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),hafla iliyoanza leo Disemba 4 hadi Disemba 6,2024 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

CHUO  Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeanza kutengeneza Sera na miongozo matumizi ya teknolojia ya akili mnemba ili itumike kwa faida kuliko kuwatia woga.

Hayo yamebainishwa leo Disemba 4,2024 jijini Dodoma na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Lugano Kusiluka  wakati wa kongamano la 15 la Wahitimu wa Chuo hicho,

Prof.Kusiluka amesema katika zama hizi za sasa zinazohitaji uwekezaji wa kuisoma teknolojia Chuo Kikuu Cha Dodoma wenyewe wamekuwa kinara katika eneo hilo.

“Wanachokifanya hivi sasa ni kuanza kutengeneza Sera na miongozo ya matumizi ya teknolojia hiyo ili itumike kwa faida zaidi kuliko kuwatia woga wa aina yoyote.”amesema Prof.Kusiluka

Amesema kuwa UDOM  tupo kwenye mchakato wa kuandaa miongozo inayoendana na Mazingira ya nchi yetu kwani teknolojia ya Marekani ni tofauti na ya Tanzania hivyo hatuwezi kuchukua moja kwa moja miongozo yao ni lazima tujiridhishe na hii teknolojia inayokuwa kwa kasi,

“Kwenye vyuo vikuu bado kuna majadiliano kuhusu faida na hasara yake lakini hoja imekuwa tunaitumiaje ili iweze kuleta faida,”amesema.

Na kuongeza kuwa ” Imani yangu ni kuwa hadi kufikia mkutano mkuu wa 16 wa Umoja wa Wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dodoma 2025 tutakuwa tayari umekuja na miongozo ili kusaidia nchi katika maendeleo ya teknolojia,” ameeleza Prof Kusiluka

Aidha  ametoa wito kwa Watanzania kutoichukia teknolojia bali waichukulie katika hali chanya huku wakitumia kwa faida kwani mabadiliko ya teknolojia yanakuja na changamoto zake ambazo ni vyema jamii ikaelimishwa ili isitumike na kuondoa ule Utanzania.

Amesema ukweli ni kwamba teknolojia hiyo inapendwa na inatumika na watu wengi, hivyo kusema kuwa inaachwa bila kutumika ni kujidanganya wenyewe.

Amesema jambo la kufanya ni kuangalia maeneo ambayo inaweza kusaidia kutoa taaluma lakini kuboresha kazi za wanafunzi.

“Lakini kitu kikubwa na changamoto kubwa ni je, utajuaje kama wanafunzi ama watu wanaoitumia kazi wanazowasilisha ni za kwao au zimetokana na watu wengine ama zimetengenezwa na kutumia akili mnemba,”amesema.

Amesema changamoto zinazojadiliwa nchini, zinajadiliwa pia duniani kote ambapo vyuo vikuu duniani vimeanza kutengeneza sera.

Amesema hivi sasa wao wanawataalamu wanaofundisha akili mnemba na wanacho kitivo chao cha Sayansi Kompyuta na Elimu Angavu.

Amesema kitivo hicho kina wataalaam tayari na miradi inayotumia akili mnemba.

Hata hivyo amesema  ni lazima watengeneze miongozo ambayo inaendana na mazingira ya nchi kwasababu zikitumika vizuri zinaweza kuleta faida.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwanza, Profesa Flora Fabian amesema amewasilisha mada inayohusu ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu katika kipindi cha akili Mnemba.

Katika mada hiyo alielezea ujio wa teknolojia hiyo, changamoto zake na vyuo vikuu vimejipangaje kuhakikisha wanaandaa wahitimu ambao wanakidhi katika soko la ajira.

Amesema mada hiyo imelenga kuangalia ufundishaji na ushirikiano uliopo kati ya vyuo vikuu na soko la ajira ikiwemo viwanda na sekta mbalimbali ambazo zinapokea wahitimu.

“Binadamu ndio anatengeneza akili mnemba, hivyo kazi kubwa tuliyonayo vyuoni ni kuhakikisha tunazalisha wahitimu ambao ni wafikiriaji na wabunifu ambao wanaweza kutumia hiyo akili mnemba kutatua matatizo ya kijamii,” amesema Prof. Flora.

About the author

mzalendoeditor