Featured Kitaifa

THBUB YATOA RAI KWA UMMA KUTOWAFICHA WATU WENYE ULEMAVU

Written by mzalendo

Na Rachel Kalonge, Dodoma.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imetoa rai kwa umma, kutowaficha watu wenye ulemavu kwa kuwa pamoja na hali yao bado ni binadamu na wanastahili kutambuliwa bila ya kujali hali yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali zilizopo kwenye maeneo wanayoishi juu ya vitendo vya ukatili, ubaguzi, udhalilishaji, unyanyasaji, unyanyapaaji kwa watu wenye ulemavu.

Rai hiyo imetolewa leo Disemba 3,2024 Jijini Dodoma na Mwnyekiti wa tume hiyo  Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akitoa tamko kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu ambapo kitaifa mwaka huu yamefanyika kitaifa Jijini la Dar es Salaam na kuongozwa na kauli mbiu isemayo “Kukuza uongozi wa watu wenye ulemavu kwa ajili ya Mustakabali jumuishi na endelevu”.

“Kauli mbiu hii inaikumbusha Serikali kuona umuhimu wa kuongeza jitihada za dhati kwa kutoa fursa za uongozi kwa watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki na kuongoza kikamilifu shughuli mbalimbali zikiwemo za Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii,”amesema Jaji Mst. Mwaimu.

Aidha, ameongeza kuwa THBUB inatambua jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kulinda na kutetea haki za Watu wenye Ulemavu nchini ikiwa ni pamoja na kuwateua watu wenye ulemavu kushika nafasi mbalimbali za uongozi, kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kwa  kufanya maboresho katika ujenzi wa majengo mapya ya umma ambayo yanajengwa kwa kuzingatia ufikikaji kwa makundi ya Watu wenye Ulemavu.

Mbali na hayo ameendeleea kutoa rai kwa umma, kutowaficha watu wenye ulemavu kwa kuwa pamoja na hali yao bado ni binadamu na wanastahili kutambuliwa  bila ya kujali hali yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali zilizopo kwenye maeneo wanayoishi juu ya vitendo vya ukatili, ubaguzi, udhalilishaji, unyanyasaji, unyanyapaaji kwa watu hao.

“Pia, wito unatolewa kwa wananchi kuachana na imani, mila, desturi na mitazamo potofu ambayo huwafanya watu wenye ulemavu kujiona hawakubaliki, hawawezi na hawana mchango kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla katika shughuli zinazohusu maendeleo,”amesema.

Siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu ni matokeo ya Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 47/3, 1992 ambapo ilipitishwa kuwa  Disemba 3 ya kila mwaka ni Siku ya Maadhimisho ya Watu wenye Ulemavu Duniani yakiwa yanalenga kuhamasisha jamii kutambua haki na fursa sawa na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika masuala ya maendeleo, mahitaji yao, changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kukabiliana nazo.

About the author

mzalendo