Featured Kitaifa

MHE. KATIMBA AWATAKA WATUMISHI WA DART KUTIMIZA MAJUKUMU YAO IPASAVYO

Written by mzalendo

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amewataka watumishi
wa wakala wa mabasi yaendayo haraka ‘DART’ kuhakikisha wanatimiza majukumu
kwa kufanya kazi kwa bidii na ufanisi kwani Wakala hiyo ni taswira ya nchi katika
sekta ya usafirishaji.

Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa
wakala hiyo katika Ofisi za Wakala Ubungo Maji Jijini Dar es Salaam alipofanya
ziara ya kikazi na amewasihi kufanyakazi kuzingatia miongozo na sheria zilizopo kwani watumiaji wa huduma za usafiri huo wa umma ni wananchi ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

“Wakala huu ni wakala muhimu sana na unabeba heshima kubwa sana ya nchi yetu
kwasababu tunajua Dar Es Salaam ndio sura ya nchi na watu wote wakifika wanafikia Dar Es Salaam kwa hiyo haya yaliyopo Dar Es Salaam hasa huduma za msingi kama usafiri huu wa Umma ndio yanajenga heshima ya nchi hivyo tutimize majukumu yetu kwa viwango vinavyotakiwa” amesema

Aidha, Mhe. Katimba ameupongeza Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka ‘DART’ kwa kasi ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu katika mradi wa awamu ya Pili kuelekea Mbagala na awamu ya tatu kuelekea Gongolamboto pamoja na awamu ya nne kuelekea Tegeta ambapo amesema ukamilishwaji wa miradi hiyo inaashria ongezeko la mabasi katika njia hizo na kufikia mwezi Disemba zaidi ya mabasi 500 yataingia nchini kwaajili ya kuanza kutoa huduma huku akutoa pongezi kwa mfumo mpya wa geti janja na kadi janja.

“Napenda nitoe pongezi zangu za dhati kwa jitihada zinazofanywa na DART hasa
kuanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya nauli, jitihada hizi zinaenda kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuimarisha makusanyo”Alisema Naibu Waziri.

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Wakala, Mtendaji Mkuu wa DART Dkt.
Athuman Kihamia amesema kwa sasa huduma inaendelea kutolewa kwenye Awamu ya kwanza ya Mradi kutokea Kimara hadi Kivukoni, Kimara hadi Gerezani na Kimara hadi Morocco pamoja na kwenye njia mlishi.

About the author

mzalendo