Featured Kitaifa

MKATABA UJENZI WA BARABARA YA IRINGA – MSEMBE WASAINIWA, BILIONI 142.5 KUTUMIKA

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana na Mkuu wa Mkoa Iringa, Peter Serukamba wakishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta na Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya CHICO, Li Jianzheng, Septemba 21, 2024 Mkoani Iringa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta na Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya CHICO, Li Jianzheng wakionesha mkataba wa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami mara baada ya kusaini mbele ya Viongozi na Wananchi, Septemba 21, 2024 Mkoani Iringa.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana na Mkuu wa Mkoa Iringa, Peter Serukamba wakishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa usimamizi wa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta na Mkurugenzi wa Kampuni ya Conseil Ingenierie Et Recherche Appliquee (CIRA SAS), Gbati Djagre, Septemba 21, 2024 Mkoani Iringa.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, akizungumza na viongozi na wananchi katika Uwanja wa Samora mara baada ya kushudia utiaji saini wa mikataba miwili ya ujeniz na usimamizi kati ya Wakala ya Barabara (TANROADS) na Mkandarasi Kampuni ya CHICO pamoja na Mhandisi Mshauri kampuni ya CIRA SAS wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami, Septemba 21, 2024 Mkoani Iringa.

Viongozi na Wananchi waliofika katika uwanja wa Samora kushuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ya ujenzi na usimamizi kati ya Wakala ya Barabara (TANROADS) na Mkandarasi Kampuni ya CHICO pamoja na Mhandisi Mshauri Kampuni ya CIRA SAS kwa kushirikiana na NIMETA Consult wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami, Septemba 21, 2024 Mkoani Iringa.

…………

Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe inayoelekea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (km 104) kwa kiwango cha lami utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 142.56 ili kufungua fursa za kiutalii, kiuchumi na kibiashara kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Utiaji saini mikataba miwili kati ya Wakala ya Barabara (TANROADS) na Mkandarasi wa Ujenzi pamoja na Mhandisi Mshauri umefanyika leo Septemba 21, 2024 katika Uwanja wa Samora Mkoani Iringa na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile pamoja na viongozi wa CCM, Serikali na Wananchi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba.

Akizungumza na wananchi, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) kuhakikisha anamsimamia Mkandarasi kampuni ya  CHICO aliyeshinda zabuni, kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa ubora na viwango na kukamilisha kazi ndani ya muda kwa mujibu wa mkataba.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua barabara hii ikijengwa itafungua fursa za Kiuchumi na Kitalii kwa wana Iringa na ametoa fedha maalum kiasi cha shilingi Bilioni 142.56 ambayo itawezesha barabara kuanza kujengwa mpaka kukamilika fedha inatiririka tu“, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameitaja mikakati ya Serikali kwa Mkoa wa Iringa ikiwa ni kuanza manunuzi kwa ajili ya kujenga barabara ya mchepuo ya Iringa – Iringa Bypass (km 7.3) pamoja na kuendelea na upanuzi wa mlima kitonga ambapo tayari kazi inaendelea katika kona 5 hatarishi na ujenzi umefikia asilimia 65.

Vilevile, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuunganisha Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa barabara za lami ili kuboresha miundombinu ya usafiri, kurahisisha biashara, na kukuza uchumi.

Kwa upande wake Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera na Uratibu William Lukuvi, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe ukikamilika kwa kiwango cha lami utafungua uchumi wa wananchi wa Iringa kwa kuwa tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli na hivyo wananchi watashuhudia makampuni mengi ya kitalii yakiongezeka. 

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa kukamilika kujengwa kwa barabara ya Iringa –  Msembe utasaidia kukuza utalii wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hasa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kurahisisha ufikaji wa watalii katika hifadhi hiyo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba ameiomba Serikali kushughulikia mapema suala la fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami ili isiwe kikwazo katika mradi huo.

Akitoa taarifa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta amezitaja Kampuni zilizoshinda zabuni za ujenzi ambazo ni China Henan International Corperation (CHICO) pamoja na Mhandisi Mshauri Conseil Ingenierie Et Recherche Appliquee (CIRA SAS) ya Mali kwa kushirikiana na NIMETA Consult ya Tanzania ambapo utekelezaji wake ni miezi 24.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuharakishamaendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Iringa hususani katika Wilaya za Iringa mjini na Iringa vijijini kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya Usafiri na Utalii.

About the author

mzalendoeditor