Featured Kitaifa

HALMASHAURI TEKELEZENI MAAGIZO YA RAIS SAMIA- MHE.KATIMBA

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amezitaka halmashauri nchini kufuata maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutenga wodi maalum ya watoto wachanga na wanaozaliwa kabla ya wakati(njiti) ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo mkoani Kigoma akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa katika ziara ya kikazi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko aliyewasili Septemba 18,2024 ambapo ameanza kwa kutembelea hospitali ya Halmashauri ya Kakonko mkoa wa Kigoma.

“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu umeweza kujionea jengo la watoto wachanga pamoja na watoto njiti na mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahususi kwamba hospitali zetu zote za Halmashauri ziwe na jengo kwaajili ya kuhudumia watoto wachanga na watoto njiti na jitihada hizi zinalenga kupunguza vifo vya watoto wachanga” Amesema

Akizungumzia kuhusu takwimu za kukabiliana na vifo kwa mama wajawazito na watoto, Mhe. Katimba amesema serikali imejenga majengo ya wazazi (Maternity Complex) wodi za watoto wachanga ambazo zimesaidia kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi kutoka vifo 556 mpaka 104 katika vizazi hao 100,000 huku Takwimu za vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja vikipungua kutoka vifo 43 mpaka 33 katika vizazi hai 1000.

Akizungumzia mafanikio hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko amepongeza uwepo wa majengo hayo ambayo yamekuwa yakiwekewa mazingira rafiki kwa afya na ukuaji wa mtoto katika hospitali za Halmashauri ikiwemo hospitali ya Halmashauri ya Kakonko.

Dkt. Biteko yupo mkoani Kigoma na ameanza ziara ya kikazi ya siku mbili na anatarajia kukagua na kuzindua miradi inayotekeleza na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

About the author

mzalendo