Featured Kitaifa

MAJADILIANO YA AWALI UTEKELEZAJI MAKUBALIANO YA MASHIRIKIANO BAINA YA GST NA GTK YAANZA RASMI

Written by mzalendoeditor

● *Dar es Salaaam*

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Ndg. Msafiri Mbibo ameongoza kikao cha majadiliano ya awali kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano ya mashirikiano (MoU) baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Miamba ya Finland (GTK) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Madini zilizopo Jijini Dar es Salaaam.

Kikao hicho kililenga kujadili namna bora ya utekelezaji wa mashirikiano hayo ambayo yalisainiwa na taasisi hizo mbili Machi 21, 2024.

Akizungumza katika majadiliano hayo yaliyoshirikisha wataalam kutoka GST na GTK, Mbibo alisema kuwa Wizara ya Madini inatambua mchango wa Finland katika mashirikiano ya utafiti, hivyo tayari imeandaa mazingira rafiki ili kuhakikisha utekelezaji unafanikiwa kama ilivyopangwa.

Aidha, Mbibo alizitaka Taasisi hizo mbili kuweka mpango wa utekelezaji na kufanya tafiti zaidi ya zile za Madini ikiwamo kubaini miamba inayo hifadhi vyanzo vya maji safi. Pia, Mbibo alisisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya mashirikiano baina ya taasisi hizo mbili.

Pamoja na mambo mengine, Mbibo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha GTK kushiriki kwenye Mkutano wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini “Mining Investment Forum” utakaofanyika Novemba 2024 Jijini Dar es salaam.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt Mussa Budeba aliainisha maeneo ya Mashirikiano ambapo alisema ni pamoja na kufanya utafiti wa jiolojia, kujengeana uwezo katika nyanja za Jiosayansi na pia kufanya tafiti za pamoja za Jiosayansi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa GTK Prof. Kimmo Tiilakainen alimueleza Naibu Katibu Mkuu kuwa GTK iko tayari kutekeleza makubaliano hayo kwa kubaini maeneo machache ya kuanzia ili kuleta tija kwa haraka.

Sambamba na hayo, Prof. Kimmo alisema, GTK ina imani na Tanzania kutokana na mashirikiano yaliyoleta mafanikio makubwa kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo Sekta ya Madini.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia Dkt. Ronald Massawe na Mkurugenzi wa Shughuli za Kimataifa wa TGK Philipp Schmidt.

About the author

mzalendoeditor