-_Azindua rasmi Chama cha Watoa Huduma na Wauzaji wa Bidhaa Migodini_
-_Afurahishwa na Watanzania kuzingatia ubora_
-_Awataka kushirikiana na kusaidiana_
-_Rais Samia apongezwa kuvutia uwekezaji_
DAR ES SALAAM: Waziri wa Madini Anthony Mavunde, amewataka watanzania wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya madini kuchangamkia fursa kubwa iliyopo ya manunuzi ya bidhaa na utoaji huduma migodini ambayo kwa mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya kiasi cha sh Trilioni 3.1 zimetumika katika eneo la manunuzi ya bidhaa na huduma.
Waziri Mavunde ameyasema hayo jana Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Watoa Huduma na Wasambazaji wa bidhaa Migodini (TAMISA).
Amesema, uwekezaji nchini Tanzania kwenye sekta ya madini unakua siku hadi siku na hii inatokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
“Chama hichi kitasaidia kuwa na sauti ya pamoja katika kuwajengea uwezo watanzania na kuwaimarisha ili kuwa shindani katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa migodini,” amesema Mavunde na kuongeza
“Natamani sana kuziona hizi Sh Trilioni 3.1 zinabaki mikononi mwa watanzania ili kuchochea uchumi wa nchi yetu kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa na huduma zenye mahitaji makubwa migodini,” amesema.
Aidha, amewapongeza TAMISA kwa kupokea na kuyafanyia kazi maagizo yangu ya uanzishwaji wa chama hichi cha watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa migodini,ni mategemeo yangu kwamba mtakuwa jukwaa zuri la mafanikio ya sekta binafsi Tanzania, “alisema Mavunde
Akitoa maelezo ya awali,Mwenyekiti wa TAMISA Peter Kumalilwa amesema chama hichi kina malengo mahsusi ya kuwaleta pamoja watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa migodini,kuishauri serikali namna bora ya kuwajengea uwezo watanzania kunufaika na sekta ya madini na kushirikiana na serikali kutatua matatizo ya msingi kwenye suala la ‘Local content’
Akitoa salamu za sekta binafsi,Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi TPSF ; na Mwenyekiti wa Kongani ya Huduma ( Service Cluster) Octavian Mshiu amepongeza hatua ambazo serikali inazichukua kwa sasa kuvutia uwekezaji na kukuza sekta binafsi nchini na kuahidi kwamba TPSF itakuwa bega kwa bega na wadau wote kuhakikisha watanzania wanachangamkia uchumi wa madini.