Featured Kitaifa

SERIKALI YATAKA WANANCHI KUSHIRIKI KUHIFADHI TABAKA LA OZONI

Written by mzalendoeditor

….

SERIKALI  imewataka wananchi kushiriki katika kuhifadhi Tabaka la Ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba). 

Pia, imewataka kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni au kusababisha ongezeko la joto duniani. 

Hayo yamesemwa leo Septemba 14,2024 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji wakati akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni ambayo yanatarajiwa kufanyika Septemba 16,2024. 

Amesema kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imepanga kutoa elimu kwa mafundi wa viyoyozi na majokofu katika jiji la Dodoma kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kuhusu namna bora ya kukarabati vifaa hivyo pasipo kuachia angani kemikali na hivyo kuharibu mazingira.

Waziri Kijaji amesema kupitia maadhimisho hayo pia wataendelea kutoa elimu kwa umma kupitia makala mjongeo kuhusu umuhimu wa kulinda tabaka la Ozoni na kuendelea kuhimiza jamii kupunguza shughuli mbalimbali za kibinadamu ambazo zinasababisha mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Tabaka la Ozoni linapoharibiwa huruhusu mionzi ya jua kufika kwenye uso wa dunia na hivyo kusababisha kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi. 

“Baadhi ya kemikali hizi husababisha kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi. Kemikali hizo ni kemikali zinazotumika katika majokofu na viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku na kilimo cha maua, hifadhi ya nafaka katika maghala na kadhalika”. 

Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka huu ni Itifaki ya Montreal: Kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi” Kauli mbiu hii imechaguliwa ili kuendelea kujenga uelewa kwa umma wa namna ambavyo Itifaki ya Montreal imechangia katika hifadhi ya tabaka la Ozoni na pia kuwa nyenzo muhimu katika kuchangia jitihada za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

About the author

mzalendoeditor