Featured Kitaifa

KASEKENYA AWATAKA WAKANDARASI BARABARA YA MNIVATA – NEWALA –MASASI KUONGEZA KASI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo alipokagua eneo la Kilambo mkoani Mtwara linapotarajiwa kujengwa daraja linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa njia fupi

Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, mkoani Mtwara, Mheshimiwa Abdallah Chikota akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (Wanne kushoto) alipokagua eneo la Kilambo mkoani Mtwara linapotarajiwa kujengwa daraja linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa njia fupi.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya walipokagua eneo la Kilambo mkoani Mtwara linapotarajiwa kujengwa daraja linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa njia fupi

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akizungumza na wananchi alipokagua eneo la Kilambo mkoani Mtwara linapotarajiwa kujengwa daraja linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa njia fupi,

Muonekano wa mto Ruvuma linapotarajiwa kujengwa daraja la Kilambo linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa njia fupi.

Muonekano wa barabara ya Mnivata- Newala – Masasi (Km 160) kwa kiwango cha lami ambayo ujenzi wake unaendelea mkoani Mtwara.

PICHA NA WU

……..

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya amewataka Wakandarasi China Wu Yi na Ms China Communication wanaojenga barabara ya Mnivata- Newala – Masasi (Km 160) kwa kiwango cha lami  kuhakikisha wanajenga barabara hiyo kwa ubora uliuokusudiwa na kukamilika kwa wakati.

Akizungumza wakati alipokagua barabara hiyo Septemba 13, 2024 mkoani  Mtwara  Naibu Waziri huyo amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua uchumi wa Mkoa huo na kuwasisitiza wakazi wa Mtwara kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha ujenzi wa barabara hii unakamilika kwa wakati, hivyo ujenzi huu umegawanywa katika sehemu mbili, Mnivata- Mitesa (Km 100) ambayo inajengwa na Mkandarasi China Wu Yi na Mitesa – Masasi (Km 60) inayojengwa na Mkandarasi Ms China Communication lengo likiwa kuharakisha ujenzi huu ili kuwawezesha wananchi wa Mtwara kunufaika”, amesema Mhandisi Kasekenya.

Ametoa rai kwa wananchi watakaopata kazi katika mradi huo kufanya kazi kwa bidii na kuulinda kwa kujiepusha na vitendo vya wizi na kusisitiza umuhimu wa Wakandarasi hao kutoa fursa za ajira kwa wananchi waishio jirani na mradi huo kadri inavyowezekana.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amekagua maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Mang’amba – Msimbati (Km 35) na Madimba – Kilambo (Km 16) ambazo usanifu wa kina wa ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika na Serikali ipo katika maandalizi ya mwisho ya kupata Mkandarasi atakayejenga barabara hizo.

Aidha, amekagua eneo litakapojengwa daraja la Kilambo litakalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa njia fupi na hivyo kukuza uchumi wa Mkoa wa Mtwara na jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Kadhalika, Kasekenya maemuagiza Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Mtwara, Dhulkifu Hamdan kuhakikisha ndani ya kipindi cha siku 10 kivuko cha Kilambo kinarejea kutoka katika matengenezo na kuendelea kutoa huduma kwenye eneo la Kilambo mkoani humo.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mtwara, Mhandisi, Dotto John amesema TANROADS mkoa huo wamejipanga kuhakikisha barabara zote zinazojengwa mkoani humo zinasimamiwa kikamilifu ili thamani ya fedha iwiane na ubora.

Naibu Waziri Kasekenya anaendelea na ziara yake ya siku Tano katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo anakagua miundombinu ya barabara na madaraja.

About the author

mzalendoeditor