Featured Kitaifa

UJUMBE WA THBUB WATEMBELEA GEREZA KUU LA BUTIMBA MWANZA

Written by mzalendo

Mfawidhi wa Ofisi ya THBUB tawi la Mwanza Bw. Gordian Binamungu (wa tatu kushoto) akikabidhi Redio kwa uongozi wa Gereza Kuu la Butimba tarehe 11 Septemba, 2024.

Na Mwandishi Wetu.

Leo tarehe 11 Septemba, 2024 Ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ukiongozwa na Bw. Gordian Binamungu, Mfawidhi wa Ofisi ya THBUB tawi la Mwanza imetembelea Gereza Kuu la Butimba lilipo Jijini Mwanza.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kukabidhi Redio na kuwalipia King’amuzi ikiwaa ni kutimiza ahadi iliyotolewa na Mwenyekiti wa THBUB Mhe. Mathew P. M Mwaimu (Jaji Mstaafu) mnamo tarehe 7 Julai, 2024 wakati alipofanya ziara ya kukagua uzingatiaji wa haki za binadamu katika Gereza hilo.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa na Bw. Gordian Binamungu kwa niaba ya Mwenyekiti wa THBUB Mhe. Mathew P. M . Mwaimu (Jaji mstaafu).

Awali katika mkutano wa THBUB na Baraza la wafungwa na Mahabusi katika Gereza hilo, Wafungwa na Mahabusu waliiomba THBUB kuwasaidia Redio na King’amuzi ili kuwawezesha kupata taarifa kuhusu matukio mbalimbali muhimu na mambo yanayoendelea nchini hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kama ilivyoainishwaa katika Ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

THBUB inaendelea na kazi ya kukagua sehemu walimozuiliwa pamoja na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii katika mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kukuza na kulinda haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

About the author

mzalendo