Featured Kitaifa

BRELA ENDELEENI KUBORESHA HUDUMA ZA USAJILI WA MAKAMPUNI NA BIASHARA NDOGO.

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo(Mb.) amepongeza kasi ya utendaji ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kufanikiwa kusajili makampuni 205507, majina ya biashara 561,014, alama za biashara na huduma 88248, viwanda 8074 na hataza 627.5. kwa kipindi cha miaka miwili.

Vile vile amewataka wabunifu wote nchini kulinda bunifu zao kwa kuzisajili kisheria ili zisichukuliwe na watu wengine na kujinufaisha nazo bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Dkt Jafo ameyasema hayo Septemba, 09, 2024 jijini Dar es Salaam alipotembelea Ofisi za BRELA kwa lengo la ili kujionea utendaji kazi na kujifunza jinsi Wakala hiyo ambayo ni miongoni mwa Taasisi 13 zilizochini ya Wizara ya Viwanda na Biashara inavyotoa huduma za Sajili mbalimbali.

Aidha, ametoa rai kwa Watumishi wa Wakala hiyo kuwa wawezeshaji kutumia kanuni na sheria na si wakwamishaji, kuwalinda wabunifu, kujiendeleza kielimu, kushirikiana kupendana, kutunza siri za wateja, kufanya kazi kwa weledi, uaminifu, uadilifu ili kuifanya BRELA kuwa miongoni mwa Taasisi bora za usajili barani Afrika katika usajili wa Makampuni, Haki miliki na Hataza.

Aidha Dkt. Jafo aliishauri BRELA kuendelea kuboresha huduma za kusajili biashara, majina, haki za ubunifu kwa kuanzisha mfumo utakaoharakisha usajili wa biashara ndogo na viwanda vidogo pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya BRELA na Taasisi zingine zinazofanya kazi kwa karibu hususan Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuongeza ufanisi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi BRELA, Profesa Neema Mori, alisema wamepokea maelekezo hayo na watayafanyia kazi kwa kuyawekea mikakati kwa kushirikiana na menejimenti ili kuhakikisha BRELA inafanya kazi kwa ufanisi kwa kusajili makampuni kwa siku tatu na wateja kupata huduma bora na kwa wakati.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema Wakala hiyo, imejipanga kikamilifu kuhakikisha inahudumia wateja kwa kasi na kwa wakati kwa kutumia mfumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasaliano (TEHAMA).

About the author

mzalendoeditor