Featured Kitaifa

UKUSANYAJI MAPATO YA NDANI WAIMARIKA NCHINI-MAJALIWA

Written by mzalendoeditor

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge, bungeni jijini Dodoma, Septemba 6, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…….

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato nchini ambapo hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kipindi cha mwezi Julai 2024 imeendelea kuimarika.

“Jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 113.701 kimekusanywa sawa na asilimia 8 ya makisio ya mwaka 2024/2025 ya shilingi trilioni 1.356. Aidha, makusanyo halisi yameongezeka kutoka shilingi  bilioni 90.665 yaliyokusanywa kipindi kama hicho cha Julai, 2023 ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni  23.036.”

Ameyasema hayo leo (Septemba 6, 2024) wakati wa kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge, jijini Dodoma. “Ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, linachangiwa na mikakati mbalimbali inayoendelea kufanywa na Serikali.”

Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na usimamizi wa vyanzo vya mapato vilivyopo, zoezi la mara kwa mara la ufanyaji tathmini ya vyanzo vya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kwa Halmashauri zote 184.

Waziri Mkuu amesema mkakati mwingine ni kutoa elimu ya ulipaji ushuru kwa wananchi, pamoja na kuendelea kusimimamia matumizi sahihi ya Mfumo wa TAUSI wa ukusanyaji mapato pamoja na mashine za kukusanyia Mapato – POS.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema mwaka huu (2024) ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajia kutafanyika siku ya Jumatano, tarehe 27 Novemba, 2024, hivyo amewasisitiza kuwasisitiza Watanzania wote kuwa tayari na kutimiza haki yao ya Kikatiba kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika huo.

Amesema tayari uandaaji wa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa katika mamlaka za wilaya na miji, mwongozo wa elimu ya mpiga kura na mwongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa umekamilika.

“Nchi yetu imekuwa na utaratibu wa kujenga misingi ya uongozi kuanzia ngazi za chini ili kuiwezesha Serikali kuwafikia watu wake katika kutekeleza masuala mbalimbali ili kufikia azma kubwa katika kuleta maendeleo endelevu.”

Amesema maandalizi mengine ya uchaguzi yapo katika hatua za ukamilishaji ambayo yanajumuisha kutangaza orodha ya maeneo ya utawala, uhakiki wa vituo vya kupigia kura awamu ya pili na manunuzi ya vifaa vya uchaguzi. “Kwa sasa mamlaka husika zinaendelea na utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia vyombo vya habari, mabango na mitandao ya kijamii.

Kwa kuwa msingi wetu wa maendeleo unaanzia katika ngazi hii, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuhakikisha tunatumia fursa ya mikutano yetu tuwapo majimboni, wasanii na vyombo vya Habari katika kutoa hamasa ya umuhimu wa wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.”

 

About the author

mzalendoeditor