Featured Kitaifa

SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA NGOs KUKUZA UCHUMI WA TAIFA

Written by mzalendo
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko,akizungumza  wakati akifunga  Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika leo Septemba 6,2024  jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko,(hayupo pichani)   wakati akifunga  Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika leo Septemba 6,2024  jijini Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza  wakati wa kufungwa Kwa  Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika leo Septemba 6,2024  jijini Dodoma.
……
SERIKALI  imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kwa kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika hayo kwani yamekua mstari wa mbele kuchagiza juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa Taifa na maendeleo kwa ujumla.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo leo Septemba 6,2024 wakati akifunga  Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika kwa siku tatu jijini Dodoma.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa NGOs zina mchango mkubwa katika kuondoa umaskini kupitia miradi mtambuka ambapo matokeo yake ni utoaji wa ajira kwa vijana wengi na huduma mbalimbali katika kila sekta nchini.
“Serikali kupitia Wizara ya Fedha ipo katika mchakato wa kuaanda mwongozo wa  Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambao ukikamilika, bajeti ya Mashirika hayo itakua inajumuishwa kwenye bajeti kuu hivyo basi, natoa  wito kwenu kuwa mkawahudumie Watanzania kwa upendo katika sekta zote na mkawe waaminifu kwenye fedha zinazotolewa kwa ajili ya kurahisisha maisha ya Watanzania,” amesema Dkt. Biteko.
Vilevile, Dkt. Biteko ametoa rai kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuhamasisha ajenda ya matumizi ya Nishati Safi kwa wananchi ili itapofika 2034 asilima 80 wawe wanaweza kutumia nishati safi na kuondokana na magonjwa yanawakumbuka wengi kwa kutumia nishati zinazowaathiri.
Kwa  upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema, kupitia uchambuzi wa taarifa za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 1,368, imebainika kuwa jumla ya Shilingi 2.6 trilioni zilipokelewa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kwamba kiasi cha Shilingi trilioni 2.4 kilitumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika nyanja mbalimbali.
“Sekta iliyoongoza kwa mwaka 2023 ilikuwa ni Sekta ya Afya, ikifuatiwa na Uwezeshaji wa Jamii Kiuchumi na Ulinzi wa Jamii. Sekta nyingine ni pamoja na Uhifadhi wa Mazingira, Sekta ya Elimu, Sekta ya Kilimo, Utawala Bora, Sekta ya Maji, Masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu. Makundi yaliyonufaika zaidi na miradi hiyo ni wanawake ambao walifikiwa kwa takribani asilimia 47.4 na vijana ambao walifikiwa kwa takribani asilimia 30.5,” amesema Dkt. Gwajima.
Naye  Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali Jasper Makala ameishukuru Serikali kwa juhudi inazofanya za kuwawekea mazingira wezeshi katika utekelezaji wao wa majukumu.
“Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na pasina shaka kuwa Serikali yetu
inayatambua na kuyathamini Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwani kwa miaka minne mfululizo tumepata Viongozi wa Juu wakuu wa Nchi kutusikiliza na kuzungumza nasi,” amesema Makala.
Sambamba na hayo, uzinduzi wa programu ya lishe kwa watoto imezinduliwa na Shirika la World Vision ambapo shirika hilo limejidhatiti kuwa ndani ya miaka mitatu itaweza kutatua changamoto ya utapiamlo kwa kutumia afua mbalimbali ikiwemo kuwawezesha wakulima kupitia utafutaji wa mitaji na masoko.
 

About the author

mzalendo