Featured Kitaifa

WIZARA KUPIMWA KWA UTEKELEZAJI WA MWONGOZO WA UJUMUISHAJI WA JINSIA KATIKA UTUMISHI WA UMMA 

Written by mzalendo

 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi akizungumza na Wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara zote na Waratibu wa Ujumuishwaji Jinsia ngazi ya Wizara wakati akifunga semina elekezi ya Mwongozo wa Jinsia katika Utumishi wa Umma.

Wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara zote na Waratibu wa Ujumuishwaji Jinsia ngazi ya Wizara wakisikiliza mada kuhusu Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Masuala ya Jinsia mahali pa Kazi wakati wa semina elekezi ya Mwongozo wa Jinsia katika Utumishi wa Umma

Wawezeshaji katika semina elekezi ya Mwongozo wa Jinsia katika Utumishi wa Umma wakijadili jambo na kupitia nyaraka zao kabla ya kuwasilisha mada kwa Wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara zote na Waratibu wa Ujumuishwaji Jinsia ngazi ya Wizara.

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bi. Nyasinde Mukono (katikati) akijadili namna ya kuandaa Mpango Kazi wa Masuala ya Jinsia Mahali pa Kazi na Mratibu wa Ujumuishwaji Jinsia ngazi ya Wizara kutoka katika ofisi hiyo Bw. Kokolo Lusanda (wa kwanza kushoto) wakati wa semina elekezi ya Mwongozo wa Jinsia katika Utumishi wa Umma iliyofanyika jijini Dodoma.

Na Veronica Mwafisi-Dodoma

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amezitaka Wizara zote kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mwongozo wa Ujumuishaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma kila mwisho wa mwaka katika Ofisi hiyo ili kuhakikisha Mwongozo huo unatekelezwa kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa na Serikali.

 

Bw. Daudi amezungumza hayo leo wakati akifunga semina elekezi ya siku mbili ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma kwa Wakurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara pamoja na Waratibu wa Jinsia Ngazi ya Wizara iliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema kuwasilisha taarifa ya utekelezaji na kupimwa kila mwisho wa mwaka ni suala la lazima kwani kuongea ni suala lingine na utekelezaji ni suala lingine, hivyo ni lazima wapimwe ili kuona namna mwongozo huo unavyotekelezwa kwa maslahi mapana ya taifa.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka Wakurugenzi hao na Waratibu wa Madawati ya Jinsia kutekeleza Mwongozo huo kwa kushirikiana na Idara na Vitengo vilivyo ndani ya Wizara zao kwani ukiwa shirikishi utekelezaji wake unakuwa ni rahisi na wa haraka.

Vile vile amezielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara zote kutekeleza Mwongozo huo kupitia Wakurugenzi hao ambao ni wawakilishi kwa sababu Serikali haitoweza kumwita kila mmoja na kutoa semina hiyo.

“Sasa haya ni maelekezo, kwasababau sisi hatuna uwezo wa kumwita kila mmoja mahali hapa, ninyi ni wawakilishi wenye nguvu kubwa, hivyo haya tunayoyasema mahali hapa mkiyafikisha kwa wenzetu wa taasisi, itakuwa jambo jema kwani kwa kufanya hivyo Serikali itatekeleza mambo yake kwa ufanisi mkubwa” 

Semina elekezi ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma kwa Wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara zote na Waratibu wa Ujumuishwaji Jinsia ngazi ya Wizara imefanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 2 hadi 3 Septemba, 2024 katika Ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha jijini Dodoma.

About the author

mzalendo