Featured Kitaifa

WAKANDARASI MIRADI YA UJENZI YA HEET UDOM WAASWA

Written by mzalendo

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka Wakandarasi walioshinda Zabuni ya Ujenzi wa Majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kuzingatia ubora katika ujenzi wa Majengo hayo na kukamilisha kwa wakati.

Hayo amesema , katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya uj enzi wa Majengo ya Madarasa na Maabara iliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

“Sisi kama Mkoa tunachukulia UDOM kama Chuo cha pekee na ni Chuo ambacho tunajivunia, niwasisitize  Wakandarasi kuwa mmejenga hoja kwenye makaratasi, mkaaminiwa, tuonyesheni kwa vitendo kuwa mnafaa kuaminiwa” Alisisitiza  Senyamule

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Rwekaza Sympo Mukandala, amesema kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza ubora wa miundombinu ambao utapelekea mageuzi makubwa katika utoaji wa taaluma bora nchini.

Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka, amesema kutokana na ujenzi wa majengo hayo, UDOM itaongeza idadi ya wanafunzi ambao ni mpango wa muda mrefu wa  serikali wa kuhakikisha UDOM inakuwa na uwezo wa kusajili wanafunzi zaidi ya 40,000 kwa mwaka.

Akizungumzia Mratibu, Mratibu wa mradi huo UDOM ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina, amesema mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano na utakamilika mwaka 2026, kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa masharti nafuu toka Benki ya Dunia.

Aidha, alieleza lengo la mradi huo ni kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kuwianisha mitaala na soko la ajira katika programu za kipaumbele katika taasisi za Elimu ya Juu, na kuboresha usimamizi wa mfumo wa Elimu ya Juu kwa ujumla.

Alieleza pia kuwa Mradi huu unatekelezwa katika maeneo mbalimbali hapa UDOM ikiwa ni pamoja na kuanzisha kampasi mpya mkoa Njombe, kuboresha matumizi ya TEHAMA, kuhuisha mitaala inayozingatia mahitaji ya soko pamoja na kuongezea ujuzi wahadhiri kwa ngazi mbalimbali za masomo.

Utiaji saini wa Mikataba hiyo ulifanyika kati ya Chuo Kikuu cha Dodoma na M/S DEMATOCLASA REALHOPE JV MPONELA CONSTRUCTION AND COMPANY LTD ambayo itajenga jengo la madarasa katika Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi na M/S CHINA ENERGY ENGINEERING GROUP JIANGSU NO.1 ELECTRIC POWER CONSTRUCTION CO. LTD itakayojenga jengo la Maabara ya kisasa katika Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati.

Hafla hiyo ilihudhuria na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya UDOM wakiwemo Mkuu wa Wilaya Dodoma Mjini, Wajumbe wa Baraza la Chuo, Menejimenti ya Chuo, Viongozi wa kijiji cha Ng’hong’hona na Viongozi wa Vyama Vya Wafanyakazi na Wanafunzi UDOM.

About the author

mzalendo