Featured Kitaifa

SERIKALI KUWEKA CHUMBA MAALUM SHULENI KWA WANAFUNZI WA KIKE KUJISITIRI WAKATI WA HEDHI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma. 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Zainab Katimba amesema Serikali itaendelea kuzingatia suala la usiri wa ugawaji wa taulo za kike mashuleni na vyuoni kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na chumba maalum shuleni kwa wanafunzi wa kike kujisitiri wakati wa hedhi.

Mhe. Katimba ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Magomeni Mwanakhamis Said aliyetaka kujua kama Serikali haioni haja ya kuweka usiri wa ugawaji wa taulo za kike mashuleni na vyuoni ili kudumisha silka na utamaduni wa Mtanzania.

“Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatambua vyema mila, desturi na utamaduni wa nchi yetu kuhusu suala la hedhi salama”amesema.

Pia ameongeza kuwa Utafiti uliofanywa na NIMR mwaka 2021 ulibaini kwa kiasi kikubwa wanafunzi wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo kutokana na ukosefu wa bidhaa za hedhi kwa siku 5 hadi 7 kwa mwezi sawa na siku 50 au 70 kwa muda wa masomo.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaweka jitihada kuhakikisha jamii inatambua umuhimu wa hedhi salama na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya hedhi kwa wasichana”,ameongeza.

Lengo ni kuwezesha uwepo wa vifaa sahihi vya kujisitiri, upatikanaji wa maji safi na sabuni pamoja na sehenu sahihi ya kuhifadhia / kutupa vifaa ambavyo tayari vimetumika.

About the author

mzalendo