Featured Kitaifa

AMAMA FARMS LTD MBANGUAJI BORA WA KOROSHO KWA MWAKA 2023/ 2024

Written by mzalendo

Na MwandishiWetu, Dodoma.

Amama Farms Limited yaibuka na tuzo ya mbaguaji bora wa korosho katika kundi la wabanguaji wakubwa wa korosho kwa mwaka 2023/ 2024.

Tuzo hiyo imetolewa katika mkutano  Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho wa siku mbili ulioanza Julai 22, 2024 na kutamatika Julai 23, 2024 jijini Dodoma.

Mkutano huo mkuu ulitamatika kwa mjadala wa pamoja ukifuatiwa na tuzo mbali mbali zilizotolewa ambapo Amama Farms Limited iliibuka kidedea kwa kunyakua tuzo ya kundi bora la mbanguaji mkubwa wa korosho kwa msimu wa mwaka huu.

Kiwanda cha Amama kilianza shughuli (kuanzisha tena kiwanda) mnamo mwaka 2022, kikiwa na lengo la kuongeza thamani ya mazao ya chakula ya ndani na kubadilisha kilimo cha Tanzania kutoka kuwa muuzaji wa malighafi yenye thamani ya chini hadi kuwa sekta ya mauzo ya nje ya bidhaa zilizosindikwa zenye ubora wa juu.

Kiwanda hicho kinapatikana Tandahimba, mji mdogo Kusini mwa Tanzania karibu na mpaka wa Msumbiji ikiwa ni kiwanda pekee cha kubangua korosho katika eneo hilo, sehemu ya kipekee kwa kubadilishana ujuzi, taarifa, msaada na matumaini ya siku za usoni.

Akipokea tuzo hiyo katika hitimisho la mkutano huo Bwn. Willem Warmenhoven amesema, “ ni furaha kwangu pamoja na familia ya Amama Farms Ltd, tuzo hii sio kwa Amama tu, ni kwa niaba ya wabanguaji wote humu, kwani tuzo hii ni chachu ya uchapaji kazi na mimi sipaswi kuzungumza yote haya lakini tunaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani wamekuwa msaada mkubwa katika kutoa ushauri na kushirikiana na kampuni za korosho”.

Warmenhoven hakuficha kusema kuwa Korosho za Tanzania ni moja ya zao bora kulinganisha na za nchi nyengine kwani zina ladha tamu na kubwa , pia ameeleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni moja ya changamoto wanazokumbana nazo katika zao hilo la korosho.

Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji Hussein Bashe akiwa mgeni rasmi katika mkutano huo mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka ndani na kuwafungulia mashitaka viongozi wa Vyama vikuu vya ushirika na Viongozi wa maghala ambao wanajihusisha na uhujumu wa zao la korosho nchini.

Waziri Bashe amewaambia wajumbe wa mkutano huo, “nilipata aibu pale nilipopokea mgeni kutoka nchini India, ambaye alinifuata bungeni wakati wa vikao vya Bajeti akinilalamikia kwamba ameuziwa Korosho kutoka Tanzania ambazo hazifai zimebadilika hata rangi, kama zao hilo mtaendelea kulifanya hivyo huenda mkaliua siku si nyingi, sitakubali watu wachache waliue zao hili hivyo mimi na wao mpaka kieleweke”.

About the author

mzalendo