Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI SANGU AWAASA WATUMISHI WA SEKRETARIETI YA AJIRA KUWAJIBIKA

Written by mzalendo

Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amewaasa Watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuwajibika kwa viwango vikubwa katika kutekeleza majukumu yao ili kutimiza azma ya taasisi hiyo katika kutoa ajira kwa kutenda haki sawa kwa kila mwananchi.

Mhe. Sangu ameyasema hayo leo tarehe 22 Agosti, 2024 wakati alifanya ziara yake ya kikazi iliyolenga kujifunza majukumu ya ofisi hiyo na kuhimiza uwajibikaji.

“Niwaase kuwajibika kwa viwango vikubwa katika kutekeleza majukumu yenu hasa kwa kutenda haki sawa kwa kila mwananchi atakayeomba ajira, zingatieni maadili ya taasisi hii kwa maslahi ya taifa, amesema Mhe. Sangu”.

Aidha, Mhe. Sangu ameipongeza Menejimenti ya Sekretarieti ya Ajira kwa kuboresha na kurahisisha usaili kwa kutumia TEHAMA kwani haki inatendeka na inaijengea taasisi uaminifu mkubwa kutoka kwa wananchi.

Mhe. Sangu ameendelea na ratiba yake ya kutembelea taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kujifunza kuhusu majukumu ya taasisi hizo na kuhimiza uwajibikaji.

About the author

mzalendo