Featured Kitaifa

WAKAZI WA MLIMBA WASHAURIWA KUTUMIA TAASISI ZILIZO RASMI KUPATA HUDUMA ZA FEDHA

Written by mzalendoeditor
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro Bi. Neuster Ngelela, akiongea na wananchi wa Halmashauri hiyo (hawapo pichani) wakati wa kufunga program maalum ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Na. Ramadhan Kissimba, WF, Morogoro
 
Wakazi wa Halmashauri ya Mlimba, Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro wametakiwa kuhakikisha wanatumia Taasisi za huduma ndogo za fedha ambazo zimeidhinishwa kisheria kufanya shughuli hizo nchini kwa mujibu wa Sheria.
 
Akizungumza katika program ya elimu ya fedha inayoendeshwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Fedha nchini, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba Neuster Ngelela, alisema kuwa ili kupunguza migogoro kati ya wananchi na watoa huduma ndogo za fedha ni vyema wananchi wakajielekeza kupata huduma hizo katika Taasisi za fedha zilizo rasmi na zilizosajiliwa na kupewa leseni ya kuendesha shughuli hizo.
 
Bi. Ngelela alisema kuwa kutokana na kasi ya maendeleo nchini kila mtu amekuwa na uhitaji mkubwa wa pesa, hivyo kuwasihi wananchi wa Halmashauri ya Mlimba na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha pesa wanazozipata wanazitunza kwa ajili ya maisha ya baadae na hata wakiamua kukopa basi wakope kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
 
‘’Katika maisha ya sasa kila jambo ni pesa hivyo ni vyema kila anayehitaji kupata huduma ya fedha iwe ni kukopa au kuwekeza ni vyema akaenda kupata huduma hizo katika Taasisi zilizosajiwa kutoa huduma hizo ili hata ikitokea mgogoro iwe rahisi mwananchi kupata haki yake, kwani Serikali haipendi wananchi wake waingie kwenye migogoro itakayowapotezea muda wa uzalishaji mali’’ alisema Bi. Ngelela.
 
Aidha, Bi.Ngeleja alitoa wito kwa wananchi wote wa Halmashauri ya Mlimba na vitongoji vyake kujitokeza kwa wingi ili kupata elimu kuhusu masuala ya fedha, uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi, elimu ambayo itawasaidia katika kufanya maamuzi ya matumizi sahihi ya kipato wanachokipata kutokana na uzalishaji wa mazao mbalimbali yanayolimwa katika Halmashauri hiyo.
 
Akiongea katika program hiyo, Diwani wa Viti Maalum wa Halmashauri ya Mlimba, Mhe. Reniter Limba aliwashukuru waratibu wa program kwa elimu waliyoitoa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine itasaidia kupunguza wimbi la utapeli lililokuwa linafanywa na watoa huduma za fedha ambao si waaminifu kwa kutoa mikopo yenye riba kubwa na kusababisha wananchi washindwe  kurejesha na kuleta taharuki katika familia.
 
Mhe. Limba, aliongeza kuwa njia ya kisasa iliyotumiwa na timu ya program ya elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha ya kutumia filamu kutoa elimu hiyo imewavutia wengi na kuahidi kuisambaza filamu hiyo kwa wananchi wengi zaidi ili kila mwana Mlimba na wananchi wote wa Wilaya ya Kilombero wafaidike na elimu hiyo.
 
Program ya kutoa elimu ya Fedha kwa Umma imeandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Fedha nchini ikiwa ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21-2029/30.
 
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro Bi. Neuster Ngelela, akiongea na wananchi wa Halmashauri hiyo (hawapo pichani) wakati wa kufunga program maalum ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
 
 
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro Bi. Neuster Ngelela, akishauriana jambon a Afisa Usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya katika program ya elimu ya fedha iliyotolewa katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mlimba, Wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro.
 
 
Diwani wa Viti Maalum wa Halmashuri ya Mlimba, Mhe. Reniter Limba, akiongea na wananchi wa Halmashauri hiyo (hawapo pichani) wakati wa kufunga program maalum ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo. Nyuma ya Mhe. Diwani ni Mkuu wa Divisheni ya Afisa Maendeleo ya Jamii – Halmashari ya Mlimba, Bw. Sebastian Kaole.
 
 
Afisa usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akiongea na wananchi wa Halmashauri hiyo (hawapo pichani) wakati wa kufunga program maalum ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
 
 
Mratibu wa Mifuko na Program za Uwezeshaji, kutoka Baraza la  Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bw. Samwel Shikona, akieleza kuhusu fursa za kuwawezesha wananchi kiuchumi zinazotolewa na Baraza hilo wakati wa program ya elimu ya Fedha iliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
 
 
Mratibu wa Program ya Elimu ya Fedha kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Gibson Mwakoba, akifafanua jambo kwa wananchi waliohudhuria program ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
 
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha, Morogoro)

About the author

mzalendoeditor