Featured Michezo

MASHINDANO YA UTAMADUNI YA MKUU WA MAJESHI NCHINI YATIMUA VUMBI JIJINI DAR ES SALAAM.

Written by mzalendo

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma,akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa   mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi Msasani Beach Jijini Dar es salaam.

……

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma amefungua mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi ambapo amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hususani Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Jacob John Mkunda kwa kuja na wazo la kuwa na mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi (CDF Cultural Competition).

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo Msasani Beach Jijini Dar es salaam Agosti 19 2024 Mhe. Mwinjuma amesema Jeshi limetekeleza kwa vitendo maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu kuwa kila mmoja ana wajibu wa kupenda, kuenzi na kuendeleza utamaduni wetu.

“Nimefurahi sana kusikia kuwa mashindano haya yatakuwa yanafanyika kila mwaka lakini kwa mwaka huu ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 60 ya Jeshi letu. Jambo hili ni la msingi sana kwa uhai wa taifa letu na ukweli Jeshi limeandika historia kubwa ”

Mhe. Mwinjuma ameonesha kupendezwa na mwamko wa vikundi vya sanaa vya Jeshi kushiriki mashindano hayo pia ambavyo jeshi limeweza kuwa na bendi na vikundi vya ngoma vingi ambavyo kipekee vinadumisha na kuendeleza utamaduni.

“Kufanyika kwa mashindano haya kwetu imekuwa ni faraja kubwa, niahidi hapa kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Dkt.Damas Ndumbaro kuwa Wizara itatoa kila aina ya msaada unaotakiwa kuhakikisha mashindano haya muhimu yanafanikiwa”

About the author

mzalendo