Featured Kitaifa

BILIONI 43 ZATEKELEZA MIRADI WILAYA YA HAI

Written by mzalendo

Na Mwandishi wetu – Kilimanjaro

Imeelezwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni 43 zimetolewa na Rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro.

Hayo yameelezwa na Mbunge wa Viti Maalum Kundi la Wenye Ulemavu na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tarafa ya Lyamungo mara baada ya kutembelea Tarafa ya Machame na Masama.

Mhe. Nderiananga alimpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuchochea maendeleo ya Jimbo na Hai na akatumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la MpigaKura ili kuwa na haki ya kuchagua kiongozi wanayemtaka katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025.

“Tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu wakati ukifika mjitokeze mjiandikishe pamoja na daftari la mkaazi sasa kupitia uchaguzi huu wa serikali za mitaa kama tunaona wanawake wanakubalika katika maeneo yao wapewe fomu wagombee bila upendeleo kwa kuzingatia uwezo wao wa kazi,” Alisema Mhe. Nderiananga.

Aidha aliendelea kuwaomba wazazi na walezi kuwapeleka watoto shule wakiwemo wenye ulemavu ikiwa ni haki yao kisheria ya kupata elimu badala ya kuwafungia ndani na kuwafanyia vitendo vya kikatili ambavyo huwaathiri kisaikolojia na kuharibu ndoto zao.

“Kuna wazazi wenye watoto wenye ulemavu au walezi niwaombe msiwafungie watoto ndani wapeni fursa wakasome kesho watasimama kama mimi Ummy ninayeongea mbele yenu kwa sababu Serikali imeweka mazingira wezeshi, wapeni imani hasa kina mama wasijione wanyonge kwa kuzaa mtoto mwenye ulemavu wakiona kama ni laana kumbe ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu hivyo tuwapende na kuwajali,”Alisistiza.

Katika hatua nyingine Mhe. Nderiananga alichangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT na mifuko mingine 50 ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kimashuku.

About the author

mzalendo