Na Mwandishi- Kilimanjaro.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka Viongozi wa Kata na Wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushirikiana kuwatambua wagonjwa waliofichwa ndani na watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kupata huduma ya afya hatimaye kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Mhe. Nderiananga alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii 170 yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Apotheker Health Access Initiative kwa kushirikiana na Taasisi ya Dkt. Godwin Mollel Mbunge wa Jimbo la siha na Naibu Waziri wa Afya ambapo alisema kila mwananchi ana haki ya kupata matibabu sahihi kwa mujibu wa sheria bila kujali hali yake ikiwa ni mwenye ulemavu au hana ulemavu huku akiwasisitiza kuwa sehemu ya faraja kwa wagonnjwa badala ya kuwanyanyapaa.
Aliwahimiza kufanya kazi kwa ushirikiano hatua itakayosaidia kuwafichuwa baadhi ya wagonjwa waliofichwa ndani na kukosa matibabu pamoja na kuisaidia jamii kwa kutoa elimu ya masuala ya afya kwa lengo la kuepukana na magonjwa mbalimbali hatimaye kuwa na jamii yenye afya bora.
“Viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii nyinyi mna jukumu kubwa sana la kuhakikisha mnavumbua wagonjwa waliofichwa, aidha wagonjwa au wenye ulemavu kwani na wao wana haki ya kupata huduma, tusiwaweke ndani watoeni ili wapate msaada kwa sababu kumfungia ndani kunahatarisha afya yake na utakuwa umemfanyia ukatili,” Alisema Mhe. Nderiananga.
Naye Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel alieleza kwamba ni muhimu kwa viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushirikiana katika kuhakikisha usalama wa afya za wananchi katika maeneo yao zinaimarika kwani wao ni watu wa karibu zaidi na jamii husika.
“Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akitoa fedha nyingi za kutekeleza miradi mikubwa ya huduma muhimu ya afya kama ujenzi wa Vituo vya Afya, hospitali za Wilaya, Mkoa na Rufaa pamoja na kutoa fedha za kununua vifaa tiba kuhakikisha wananchi wanatibiwa vizuri na kupunguza gharama ya kuwasafirisha kwenda nje ya Nchi,” Alipongeza Mhe. Dkt. Mollel.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Operesheni na Programu kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Apotheker Dkt. Angel Dillip amesema kuwa ni muda wa kuwaunganisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii na viongozi wa kata kwani wote wanafanya kazi eneo moja hivyo kurahisisha shughuli ya kuimarisha hali ya huduma za afya kwa wananchi endapo watakua pamoja.
Aidha Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo ya Biashara na Sera kutoka Apotheker Dkt. Suleiman Kimatta amewaasa viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kukabiliana na udumavu.
“Vijana balehe ni kuanzia miaka 10-19 kundi ambalo linatakiwa kuangaliwa sana hususani katika kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI, Kupunguza mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia, afya ya akili na lishe kwa watoto. Viongozi mna wajibu wa kutumia mikutano yenu kuzungumzia masuala ya afya kuijengea jamii uelewa ili kuepukana na magonjwa mbalimbali,” Alieleza Dkt. Kimatta.