Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wenye mabenki nchini kuwekeza zaidi kwa kuwafuta wakulima na wafugaji na kuwavutia kupata huduma za kibenki na kujiletea maendeleo.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Agosti 12, 2024 wakati hafla ya uzinduzi wa tawi la Benki ya KCB wilayani Geita
Amesema kuwa licha ya benki ya KCB kuvutia huduma zao kwa wafanyabiashara wavutie pia wakulima na wafugaji kwa kuwa ndilo kundi kubwa ambalo bado linakabiliwa na changamoto za huduma za mikopo katika benki mbalimbali nchini.
“ Nimefurajika kuona KCB imefungua tawi Geita na kusogeza huduma za kibenki kwa wananchi hii itasaidia kuchochea uchumi kwao na mjue mko mahali ambapo wananchi wake wanafanyakazi kwa bidii, wanalima, kufuga kwa bidii na wafanyabiashara wanafabiashara kwa bidii na wengine wako sekta ya madini,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Natoa wito kwa wafanyakazi wa KCB wapokeeni wateja wenu kwa bashasha, wapeni huduma nzuri na pia nendeni kwa wakulima na wafugaji kawasaidieni ili wapate huduma za kifedha hasa mikopo ili iwasaidie kuweza kukuza shughuli zao au biashara zao.”
Aidha, ameishukuru benki hiyo kuwekeza Geita na kusema kuwa Serikali inatekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo ambao unahitaji wadau pia kuendeleza ikiwemo sekta ya benki.
“ Serikaki imekuwa ikifanya juhudi ili kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwepo bima, dhamana na mifuko ya uwezeshaji na ubora wa huduma za kibenki ili kuendelea kuwasogezea huduma wananchi na sasa kiwango cha mikopo chechefu kimepungua kwa kuwa mikopo hiyo ni hatari naipongeza Benki Kuu na wakopaji kwa kujua umuhimu mikopo,” amesema Dkt. Biteko.
Pamoja na mafanikio mengine Dkt. Biteko ameipongeza KCB kushirikiana na Serikali katika matukio mbalimbali ikiwemo msaada wake wa shilingi milioni 125 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa maafa ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere mwaka 2018.
Aidha, amesema KCB imeshirikiana katika utoaji wa mikopo kwa ajili ya utelekezaji miradi ya maendeleo katika sekta za nishati, maji na miundombinu.
” KCB imetoa zaidi ya shilingi bilioni 329.7 kwa Wakala wa Nishati Vijini (REA) ambazo wamekopa wakandarasi ili kupeleka umeme vijijini ambapo umefikia asilimia 95, shilingi bilioni 107.1 kwa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na kutoa shilingi bilioni 103.9 kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali, amesema Dkt. Biteko
Naye, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema KCB ni moja ya benki zinazofanya vizuri katika sekta ya fedha nchini na imeendelea kusaidia kutimiza azma ya Serikali ya kuwekeka uchumi jumuishi nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya shughuli za kiuchumi nchini na kusema tawi la KCB kufunguliwa katika Mkoa wa Geita ni kwa sababu wameangalia shughuli za kiuchumi na mzunguko wa fedha na kuwa anawapongeza wananchi wa Geita kwa kuendelea na shughuli za kiuchumi.
“ Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia tumezalisha kilo 53,000 za dhahabu kutoka Geita Gold Mine pamoja na wachimbaji wadogo na wameuza dhahabu hizo nje ya nchi na fedha hizo zinarudi hapa kwetu hivyo niwapongeze KCB benki kwa kuja kutufungua tawi h
Vilevile, Mkurugenzi wa Kanda wa Biashara na Mkuu wa KCB Benki Tanzania, Cosmas Kimario amesema kuwa benki hiyo imeendelea kukua na kuendeleza uwekezaji wake wa biashara za kibenki katika maeneo mbalimbali nchini na kuwa sasa ina zaidi ya miaka 25 na matawi 17.
“ Tumeamua kuja Geita na kuendelea kupanua huduma za kibenki Tanzania kwa sababu ya mazingira wezeshi. Namshukuru Rais Dkt. Samia na Serikali kwa ujumla kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na tumeweza kupanuka na kuongeza matawi na tutaendelea kupanua huduma zetu.” Amesema Kimario.
Ameongeza benki hiyo ni kubwa kuliko zote Afrika ya kati ambayo imeendelea kushirikiana na Serikali ili kufanikisha utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali pamoja kuwekeza zaidi huduma zao kwenye mifumo ya digitali.