Featured Kitaifa

BALOZI NCHIMBI: KAZI KUBWA ZA RAIS SAMIA ZIMEMHESHIMISHA MAGUFULI

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa kazi kubwa anayoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo namna sahihi ya kumuenzi Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.

Balozi Nchimbi amezitaja mojawapo ya kazi hizo kubwa zilizofanywa na na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuendeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya kitaifa kwa ujumla na mingine katika Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato, iliyoanzishwa wakati wa uongozi wa Rais Magufuli.

Katibu Mkuu wa CCM amesema hayo leo Jumapili Agosti 11, 2024, wakati wa sala fupi ya kumuombea Hayati Magufuli iliyofanyika kwenye kaburi la kiongozi huyo.

Vilevile, Balozi Nchimbi alirejea maneno yake hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya Zamani, mjini Chato, akitaja baadhi ya miradi, ikiwemo ujenzi wa Treni ya Kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na jinsi ambavyo Serikali inayoongozwa na Rais Samia imeshusha kiasi cha Sh. 123 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Chato.

Hapo awali, wakati wa mapokezi ya msafara wa Katibu Mkuu wa CCM ulipokuwa ukiingia Mkoa wa Geita, ukitokea mkoani Kagera, katika Kata ya Muganza, aliwasisitiza wananchi wa eneo hilo umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kama alivyokuwa Rais Magufuli, ikiwa ni mojawapo ya njia nzuri za kumuenzi.

Balozi Nchimbi amesema kuwa yeye na msafara wa viongozi, wakiwemo Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM aliombatana nao, wamefarijika kufika mahali hapo alipozikwa kiongozi huyo, ikiwa ni mojawapo ya njia ya kumuenzi kwa uongozi wake alioutoa kwa CCM na nchi kwa ujumla.

“Sote ni mashahidi na tunatambua mchango mkubwa wa Hayati Magufuli kwa Chama chetu na nchi yetu. Kazi hiyo kubwa aliyofanya iliashiria uzalendo mkubwa aliokuwa nao. Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwa kuendeleza miradi yote iliyoachwa na hayati Magufuli, ikiwemo ya Mkoa wa Geita na Chato, kama alivyosema Mbunge,; anasema na kuongeza

“Kama kuna kitu kizuri katika kumuenzi na kuendeleza kazi kubwa ya Hayati Magufuli ilikuwa ni kuendeleza na kumaliza miradi mbalimbali mikubwa. Hiyo imekuwa ni heshima kubwa kwake Hayati Magufuli, maanza imeendelezwa na kufanyiwa kazi kama ilivyokuwa ndoto zake,” amesema Balozi Nchimbi, wakati wa sala hiyo iliyoendeshwa na Padri Clian Malegeya, kaburini kwa Hayati Magufuli.

Mbali ya kuhani kaburi la Hayati Magufuli, Balozi Nchimbi pamoja na ujumbe wa viongozi wa Chama na Serikali alioambatana nao, na kuwapatia pole familia kwa msiba huo, alipata nafasi ya kumjulia hali Mama yake Hayati Magufuli, Bi. Suzana Musa Magufuli, nyumbani hapo.

Balozi Nchimbi pamoja na msafara wake wa Wajumbe wa Kamati Kuu, Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) – Oganaizesheni, Ndugu Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Ndugu Rabia Abdalla Hamid, Katibu wa NEC – Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ameanza ziara ya siku 3 katika Mkoa wa Geita leo Agosti 11, 2024, akiwa ametokea Mkoa wa Kagera.

About the author

mzalendoeditor