Featured Kitaifa

BALOZI NCHIMBI ‘ATUMA SALAAM’ KWA BASHUNGWA, UJENZI BARABARA KIBONDO, FIDIA WANANCHI

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameiagiza Serikali kufanya malipo ya madai ya fedha anazodai mkandarasi anayejenga Barabara ya Kibondo town link, ambaye amesimama kuendelea na ujenzi, ili aendelee na kazi.

Aidha, Balozi Nchimbi, ameitaka Wizara ya Ujenzi kulipa fidia kiasi cha Shilingi 1.4 bilioni, ili wananchi wa Kibondo, Jimbo la Muhambwe, walioathiriwa na ujenzi wa barabara, waendelee na shughuli zao.

Fidia hiyo ni kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara inayoendelea kujengwa kutoka Kibondo hadi Mabamba, yenye thamani ya Sh. 60 bilioni.

Pia Dokta Nchimbi ameielekeza serikali kuhakikisha ujenzi wa miundombinu ya barabara ya Kasulu – Kibondo, inakamilika kwa wakati uliopangwa, huku pia akisisitiza wito wake kwa wanaCCM na Watanzania kwa ujumla, waendelee kujivunia na kuyatangaza mafanikio ya Serikali ya CCM, katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, yaliyofikiwa chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katibu Mkuu huyo wa CCM ametoa maelekezo hayo alipokua akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Kibondo, Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma, leo Jumanne, Agosti 6, 2024, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku tatu, Mkoa wa Kigoma.

Kupitia mkutano huo, Balozi Nchimbi amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, ahakikishe serikali inamlipa mkandarasi huyo ili aendelee na kazi, baada ya Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Dkt. Florence Samizi, kumtaarifu kuwa mjenzi yupo eneo la mradi na vifaa vyake, lakini kazi imesimama kwa kuwa hajalipwa.

Balozi Nchimbi, ambaye ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) – Oganaizesheni, Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Amos Gabriel Makalla na Katibu wa NEC – Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Hamid Abdallah, amehitimisha ziara yake ya siku 3 Mkoa wa Kigoma, kwa kuzungumza na wananchi wa Kibondo na Kakonko, kisha kuingia Mkoa wa Kagera, kuanza ziara ya siku 6 mkoani humo.

About the author

mzalendoeditor