Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeituhumu nchi jirani ya Rwanda kwa kukwamisha mfumo wa uongozaji kwa satelaiti duniani (GPS) mashariki mwa Kongo na kufanya mashambulizi ya mtandaoni “yenye lengo la uvurugaji”.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mawasiliano ya Kongo imesema, uingiliaji huo “hatari” wa GPS unaathiri uelekezaji ndege na hivyo kuhatarisha safari za ndege zinapowasili au kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma na maeneo mengine muhimu ya jimbo la Kivu Kaskazini, ikiwa ni pamoja na Beni, Butembo, Kibumba na Kanyabayonga.
Wizara hiyo imesema uchunguzi wa kiufundi uliofanywa na idara husika umethibitisha kuwa uhalifu huo ni kazi ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF).
Rwanda bado haijatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulivurugika mwaka 2021 baada ya Kinshasa kuishutumu Kigali kuwa inawaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana mashariki mwa nchi hiyo licha ya Kigali kukanusha madai hayo.
Serikali ya DRC imesema imelipeleka suala hilo kwa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), wakala maalumu wa Umoja wa Mataifa unaoratibu kanuni za anga za kimataifa.
#Chanzo cha habari ni Pars Today