Na Buhigwe, Kigoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kasulu-Kabanga-Muyama yenye urefu wa Km. 12.5, Salum Motors Transport Ltd (SAMOTA) kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa muda uliopangwa.
Mhandisi Seff ameyasema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara zilizo chini ya TARURA katika Mkoa wa Kigoma.
Mhandisi Seff amesema kuwa mkandarasi huyo anapaswa kuongeza muda wa kufanya kazi na kuhakikisha ubora wa kazi unazingatiwa na endapo itaonekana mradi huo unaendelea kusuasua basi hatosita kumchukulia hatua za kimkataba.
Aidha, Mhandisi Seff amemuagiza Mkandarasi huyo pamoja na Mhandisi Msimamizi Kampuni ya Ambicon kutatua changamoto ya upatikanaji wa kokoto zenye ubora unaotakiwa ili kazi ya uwekaji wa tabaka la lami ngumu uwe umekamilika ifikapo tarehe 31 Agosti, 2024.
Awali Mkurugenzi wa SAMOTA, Bw. Ally Abdallah ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayoipitia ni upatikanaji wa kokoto zenye ubora kwa ajili ya tabaka la juu la lami ambapo wanaendelea na upimaji wa ubora wa kokoto katika maabara na kuendelea kutafuta mwamba utakaotoa kokoto zenye ubora zaidi.