Featured Kitaifa

FANYENI UCHUNGUZI WA MACHO ANGALAU MARA MOJA KWA MWAKA

Written by mzalendo

*Na Gladys Lukindo, Dodoma*

Wananchi wameshauriwa kufanya uchunguzi wa macho angalau mara moja kwa mwaka ili kubaini kama kuna viashiria vya shambulizi la ugonjwa wa sukari katika jicho, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho, Dkt Joshua Mmbaga, ameshauri.

Dkt Mmbaga, ambaye anatoka Kliniki ya Macho ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ameyasema leo wakati akiwasilisha mada katika programu maulumu ya mafunzo maarufu kama Continues Medical Education (CME) inayotolewa kila Jumatano ikihusisha watumishi wote wa BMH.

“Ugonjwa wa kisukari ambao unasababisha kiwango cha sukari katika damu ambacho kinaharibu seli ambazo zinaenda kuharibu mishipa ya damu na kusababisha kuwa mishipa milaini hivyo kupasuka kirahisi na kusababisha kuvuja damu na kupoteza uwezo wa kuona,” amesema Dkt Mmbaga.

Dkt Mmbaga ametaja sababu za ugonjwa wa kisukari kuwa ni ulaji wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha sukari,wanga na unywaji wa kiwango kikubwa na uliopitiliza wa pombe, akisema hii inasabisha ugonjwa wa kisukari ambao baadae unaenda kushambulia jicho.

Dkt. Mmbaga ametaja dalili za ugonjwa huu kuwa ni kutokuona vizuri, kuona mawingu mawingu, kuona kama vijidudu vinaelea angani na kuona vitu katika maumbo yamebadilika au ghafla kupoteza uwezo wa kuona .

“Nashauri watu kufanya uchunguzi wa macho angalau mara moja kwa mwaka hata kama huna tatizo la sukari lakini pia watu wajihusishe na mazoezi ya viungo ili kujiweka katika hali nzuri ya kiafya.” amesema Dkt Mmbaga.

Dkt. Mmbaga ametoa wito kwa wenye matatizo wa kisukari wafike Hospitali Benjamin Mkapa wachunguze macho yao na kufata masharti ya madaktari wao na waliokutwa na tatizo hilo waanze matibabu mara moja ili kuepuka kupata madhara makubwa zaidi.

About the author

mzalendo