Featured Kitaifa

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR  ATAJA FAIDA ZA VIWANJA VYA NDEGE SEKTA YA UTALII

Written by mzalendo

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wafanyakazi na Mkandarasi wa Ujenzi wa Miradi inayojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar ( ZAA) ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kukagua miaradi ya maendeleo.

Na Masanja Mabula 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Viwanja vya ndege ni sehemu muhimu sana kwa ukuwaji wa uchumi wa Zanzibar ambayo inategemea zaidi shuhuli za utalii ambazo zinakwenda sambamba na uwepo wa miundombinu mizuri ya viwanja hivyo.

Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbali mbali inayojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibari.

Mhe. Hemed amesema kuwa viwanja vya ndege ni  milango mikuu ya nchi yoyote ile  duniani inayotumika kwa kusafirishia wageni ambao huchangia kwa kiwango kikubwa kukuwa kwa uchumi na kuongezeka kwa pato la nchi husika.

Amesema kuwa utakapokamilika ujenzi wa Miradi ya Viwanja vya ndege vya Terminal One na terminal two na eneo la biashara lililopo terminal three vitaondoa changamoto ya msongamano wa abiria wanaokaa muda mrefu kusubiri kuhudumiwa sambamba na kuongezeka kwa uwezo wa kutoa huduma bora na za haraka jambo ambalo litapelekea wageni wengi kuendelea kuitembelea Zanzibar mara kwa mara.

Makamu wa Pili wa Rais amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege kuhakikisha kila penye uwezekano wa kupatikana kwa kodi kuhakikisha kodi hio inakusanywa na kuingia Serikalini ili kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma mbali mbali za kijamii kwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikano kwa kampuni zote zinazojenga miradi mbali mbali nchini ikiwemo kampuni ya Estim Constraction Ltd  inayojenga miradi ya Viwanja vya ndege vya Zanzibar ili kuhakikisha wanakabidhi miradi hio kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia viwango na ubora wa hali ya juu.

Nae Waziri wa Ujenzi,  Mawasiliano na Usafirishaji Mhe. Dkt Khalid Salum Muhammed amesema uchumi wa Zanzibar unategemea zaidi Utalii hivyo ni lazima kuimarisha miundombinu ya kimkati ikiwemo viwanja vya ndege ili kuhakikisha Utalii unakuwa kwa kasi zaidi na pato la nchi linaongezeka kupitia wagemi wanaoingia Zanzibar.

Dkt. Khalid amesema ujenzi wa miradi hio inaendelea vizuri na hakuna changamoto yoyote hadi sasa ambayo itasabisha kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo sambamba na kuahidi kuwa uongozi wa wizara utahakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa kiwango kilichokusidiwa ili kufikia malengo ya Serikali iliyojiwekea.

Kwa upande wake mshauri elekezi kutoka kampuni ya Anova Consult Ltd Muhandisi  IBRAHIM GASPER amesema kuwa hadi sasa miradi yote inakwenda vizuri na ipo ndani ya wakati ambapo  amemuhakikishia Makamu makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  kuwa watakabidhi miradi hiyo ndani ya muda uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vya hali juu.

Gasper ameushukuru uongozi wa  Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji  pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya ndege  kwa ushirikiano mkubwa wanaowapatia jambo ambalo linawapa ari ya kufanya kazi kwa haraka na kukamilisha ujenzi huo kabla ya wakati uliopangwa kwa maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar.

Katika ziara hio Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amekagua UKARABATI WA JENGO LA TERMINAL ONE , UJENZI WA GENGO LA TERMINAL TWO pamoja NA UJENZI WA SEHEMU YA BIASHARA ILIYOPO TERMINAL THREE.

About the author

mzalendo