Featured Kitaifa

RAIS SAMIA AITAKA WIZARA YA NISHATI KUHAKIKISHA KATAVI INAPATA UMEME WA GRIDI IFIKAPO SEPTEMBA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Katavi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi (132kV) pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme vinakamilika kwa wakati ili Mkoa wa Katavi uingizwe kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Mhe. Dkt.Samia ameyasema hayo leo 13 Julai, 2024 wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 wa Tabora-Katavi na kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Inyonga ambapo ameridhika na maendeleo ya miradi hiyo.

‘’Natamani Katavi iachane kabisa na matumizi ya Majenereta ambayo ni gharama kubwa na pia kukamilika kwa miradi hii kutawawezesha wananchi wa Katavi kuutumia umeme kwa maslahi ya kiuchumi na kukuza uwekezaji, Serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza miradi hii nawaasa wananchi mchangamkie fursa zinazotokana na kuwepo kwa umeme wa kutosha na wa uhakika.” Amesema Dkt.Samia

Aidha, amepongeza kazi nzuri inayofanywa na TANESCO katika kutekeleza miradi ya umeme na kuwataka kuongeza kasi kwenye uunganishaji wa wateja pindi miradi inapokamilika.

Amesisitiza kuwa, umeme ni tegemeo kubwa kwa watu binafsi pamoja na uchumi wa viwanda na hiyo yote ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza uwepo wa umeme wa kutosha nchini.

Aliwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Mhe. Rais, Mkurugenzi Mtandaji wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema, mradi huo pindi utakapokamilika utaokoa kiasi cha takribani Bilioni 2.2 kwa mwezi kwa ajili ya mafuta yanayotumika kuendesha Mitambo ya Umeme inayotumiwa mkoani Katavi pindi tu itakapoingizwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.

About the author

mzalendo