Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AKAGUA MNARA WA MASHUJAA DODOMA

Written by mzalendo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Mnara wa Mashujaa  uliopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Julai 12.2024 ikiwa ni  maandalizi ya Siku ya Mashujaa itakayofanyika Dodoma, Julai 25, 2024Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi na amemtaka mkandarasi wa mnara huo ambaye ni Suma JKT kukamilisha ujenzi kwa viwango na ubora ifikapo Julai 22 mwaka huu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mwonekano wa maendeleo ya ujenzi wa Mnara wa Mashujaa  uliopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Julai 12.2024 ikiwa ni  maandalizi ya Siku ya Mashujaa itakayofanyika Dodoma, Julai 25, 2024.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Waziri Mkuu ahimiza Usimamizi Kuelekea Siku ya Mashujaa*

Na Mwandishi wetu-Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza ofisi yake kuhakikisha inaendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa itakayofanyika Jijini Dodoma Julai 25,2024.

Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo leo tarehe12 Julai, 2024 Jijini Dodoma wakati akikagua maendeleo ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa.

“Kwa kuwa tupo kwenye maandalizi na tunaendelea, maboresho yote yaendelee, Ofisi ya Waziri Mkuu muda wote watakuwa hapa, Maafisa, wahusika wote wawe hapa kuhakikisha kila hatua na kitu chochote kikikwama basi mawasiliano yasiwe ya kutafuta mtu akiwa mbali” amebainisha Waziri Mkuu

Aidha, Mhe. Majaliwa ameridhishwa na maandalizi katika maeneo ya ujenzi na upande wa Gwaride la Majeshi ya Ulinzi na Usalama lenye vikosi vitano ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Uhamiaji.

Vilevile, Waziri Mkuu amemtaka mkandarasi anayehusika na ujenzi wa eneo hilo kukumilisha ujenzi kwa viwango na ubora unaotakiwa.

“Msimamizi wetu wa ujenzi chini ya JKT, taarifa yenu nimeipokea na niamini mpaka tarehe 22 Julai, 2024 kila kitu kitakuwa tayari muhimu sasa tuongeze kasi ya ujenzi, tuongeze muda wa ujenzi mchana na usiku ili shughuli zote ziende vizuri na tunataka eneo hili liwe“smart” vile ambavyo itavutia” amefafanua Waziri Mkuu.

Awali akitoa maelezo kuhusu maandalizi hayo, Msanifu Mradi wa Uwanja wa Mashujaa Liberatus Mrema amesema kuwa ujenzi wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 84% na unatarajiwa kukamilika tarehe 22 Julai, 2024.

Akieleza kuhusu umuhimu wa kuadhimisha siku ya Mashujaa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa “Sherehe za mashujaa ni mahsusi zilizowekwa na nchi yetu kwa ajili kuenzi na kukumbuka mchango wa watu mbalimbali ambao wamejitolea kwa ajili ya uhai wa taifa letu”.

Dkt. Yonazi ameongeza kuwa, mashujaa hao ni watu mbalimbali ambao wamepigana vita au wametoa mchango kwa namna moja ama nyingine ili kulifanya Taifa la Tanzania kuwa namna lilivyo, kwa ulinzi wake, kwa usalama wake lakini pia kwa maendeleo ya uchumi.

About the author

mzalendo