Featured Kitaifa

TUMIENI FURSA MLIOIPATA KUPITIA DT KUTEKELEZA MALENGO YA SERIKALI – ABDULLA

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Katibu Mkuu wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mohammed Khamis Abdulla amewasihi vijana walionufaika na ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu awamu ya pili kupitia mradi wa Tanzania Digital (DT) kutumia fursa hiyo kutekeleza malengo ya Serikali hivyo lazima watambuwe kuwa Serikali imewalipia kwenda kusoma na sio mkopo.

Mhe. Abulla ameyasema hayo leo Julai 12,2024 Jijini Dodoma kwenye hafla hiyo iliyoambatana na utolewaji wa vyeti kwa wanufaika hao na kuongeza kuwa wanapaswa kuwajibika, kusoma na kila mmoja kuwa na malengo ambayo yatamuwezesha kutimiza yale wanayopaswa kutekeleza.

“Mtambue kuwa chanzo pekee cha mafanikio ni ujuzi na uzoefu hivyo basi mkasome kwa bidii na kupeperusha bendera ya taifa letu la Tanzania kwa uzalendo mkubwa na kulinda maslahi ya Taifa “,amesema.

Pia, ameongeza kuwa kwasasa Wizara inajenga vituo vya ubunifu kwenye maeneo ya Zanzibar, Dodoma, Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya, Iringa, Mtwara, Mwanza na Dar es salaam hivyo wanatarajia wakirudi waje kuwezesha vituo hivyo ambavyo vitatumika kuwawezesha vijana kuendeleza bunifu na tafiti zao katika TEHAMA ikiwemo matumizi ya teknolojia zinazoibukia.

“Nimatumaini yangu kuwa kupitia juhudi hizi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazozifanya itakuwa ni chachu pia kwa sekta binafsi kuendelea kuungana na Serikali kufanya uwekezaji kwa kukuza rasilimali ya wana TEHAMA nchini “, ameongeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa chanzo cha Diaspora kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Salvatory Mbilinyi akitoa mwogozo juu ya mambo wanayopaswa kufanya wawapo nje ya nchi amewaisitiza wanufaika wa mradi huo kutii na kufuata sheria za nchi pamoja na vyuo ambavyo wanaenda ili waweze kutimiza malengo yao kwa manufaa ya taifa, familia pamoja wao binafsi.

Sambamba na hilo amewahimiza kuwa wavumilivu na changamoto zote kipindi wapo masomoni pamoja na kulinda tamaduni za kitanzania kwa kuzingatia maadili na siyo kujisahau wanapokutana na tamaduni za nje ya nchi.

Awali akitoa salamu kwa niaba ya Benki ya Dunia Mratibu wa mradi wa Digital Tanzania (DT), Bw. Bakari amesema kupitia mradi huo wanatengeneza vituo bunifu ambavyo vitaenda kuwasaidia wanafunzi wanaomaliza vyuo pamoja na walioko mtaani kuweza kusaidiwa kuendeleza na kuonesha uwezo wao walionao.

“Vilevile kupitia mradi huu wa DT tunaenda kutengeneza mifumo ambayo kila siku Mhe. Rais amekuwa akiuongelea wa jamii namba ambapo kila mtanzania inabidi awe na namba moja ambayo itamuwezesha kupata huduma kokote aendako”,amesema.

 

About the author

mzalendo