Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam kuhusiana na Ziara ya Kiserikali ya Mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi tarehe 02 Julai, 2024.
Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam kuhusiana na Ziara yake ya Kiserikali nchini Tanzania tarehe 02 Julai, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati wakishuhudia utiaji saini Hati ya Makubaliano baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Taasisi ya Msumbiji ya Uwekezaji na Uwezeshaji Usafirishaji Nje ya Nchi, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 02 Julai, 2024. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Gilead Teri akitia saini Hati hiyo pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa AIPEX Bw. Gil Da Conceçao Bires kwa upande wa Msumbiji.
Na Sharifa B. Nyanga, Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya
Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wamekubaliana kukuza mahusiano ya kihistoria na ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Marais hao wamefikia makubaliano hayo wakati wa mazungumzo rasmi yaliyofanyika wakati wa
Ziara ya Kiserikali ya Rais Nyusi hapa nchini. Ziara hii ilianza na mapokezi rasmi yaliyofanyika
Ikulu.
Rais Samia na Rais Nyusi pia wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta ya iundombinu kama vile barabara, reli, uchumi wa buluu na anga ikiwa ni pamoja na kuanzisha safari ya ndege ya kampuni ya Air Tanzania ya moja kwa moja hadi Msumbiji.
Sekta ya miundombinu ni muhimu katika kuunganisha nchi hizi mbili na kuboresha usafiri na
usafirishaji wa bidhaa na watu ili kukuza biashara na uwekezaji.
Kwa upande mwingine, Marais hao wamekubaliana kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Huduma
cha Pamoja Mpakani ili kuweza kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji baina ya nchi mbili
hizo kupitia miradi ya pamoja na mikakati.
Tanzania na Msumbiji pia zimekubaliana kuwa na msimamo wa pamoja katika majukwaa ya
kikanda na kimataifa kama vile Jumaiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa
Afrika (AU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN)Maeneo mengine waliyokubaliana kushirikiana ni kuimarisha ulinzi na usalama katika
kukabiliana na uhalifu unaovuka mipakani.
Mbali na mazungumzo Marais hao pia walipata fursa ya kushuhudia utiaji wa saini wa Hati mbili
za Makubaliano. Hati hizo ni katika sekta ya afya inayolenga kuanzisha ushirikiano katika
kufanya utafiti, kubadilishana uzoefu na kufanya programu za pamoja za masuala ya afya
Hati nyingine ya Makubaliano ni baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Taasisi ya Msumbiji
ya Uwekezaji na Uwezeshaji Usafirishaji nje ya Nchi inayolenga kuimarisha ushirikiano na
kupanua mawanda ya biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Msumbiji.