Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI KIPANGA ASISITIZA AFYA NA USTAWI WA AKILI KUFIKIA MALENGO YA TAASISI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga akiongea na menejimenti ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Menejimenti yaliyoratibiwa na Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Elimu ya Juu (HEET ) Juni 29, 2024 kuhusu Elimu jumuishi, Afya ya Akili, Huduma kwa Wateja jijini Arusha.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula akisoma risala wakati akimkaribisha Naibu Waziri Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Menejimenti ya Taasisi hiyo yaliyoratibiwa na Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Elimu ya Juu (HEET ) Juni 29, 2024 .

Washiriki wa mafunzo ya kujengewa uwezo kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wakichangia na kufuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikitolewa na Wakufunzi mbalimbali Juni 29, 2024 .

Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga ( katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoratibiwa na Mradi HEET Juni 29, 2024.

………

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga amesisitiza Taasisi kutoa kipaumbele kwenye afya na ustawi wa akili kwa kuweka mazingira mazuri na kuhamasisha mbinu bora za kukabiliana na msongo wa mawazo ili kutokuathiri kazi, maamuzi na malengo ya muda mrefu ya Taasisi.

Mhe. Kipanga ameyasema hayo Juni 29, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Menejimenti ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela yaliyoandaliwa kwa uratibu wa na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

“Naishukuru sana Wizara kupitia mradi wa HEET na uongozi wa taasisi kwa kuona umuhimu wa mafunzo haya kwa wajumbe wa Menejimenti na kuyatoa kwa wakati” amesema Mhe. Kipanga

Kwa Upande wake Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula ameeleza kuwa, mafunzo hayo ni utekelezaji wa matakwa ya mradi wa HEET ya kuwafundisha washiriki kutambua na kuwasaidia watu wenye mahitaji maaluum, afya ya akili, jinsia, ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ili kutoa huduma bora kwa wadau.

Mradi wa HEET umejikita katika kutoa mafunzo Madhubuti kwenye masuala ya Kijinsia kwa kutengeneza Sera ya Jinsia (Gender Policy), kuunda Dawati la Jinsia (Gender Desk) pamoja na kutumia mfumo wa Serikali wa e-Mrejesho kupokea na kutuma malalamiko, pongezi pamoja na maoni.

About the author

mzalendoeditor